Marekani yaona fahari kutumiwa silaha zake haramu za vishada Ukraine
Marekani imepongeza na kusifu uamuzi wake wa kutuma mabomu yaliyopigwa marufuku kimataifa ya vishada nchini Ukraine.
Msemaji wa Usalama wa Taifa ya Ikulu ya White House ya Marekani, John Kirby jana Alkhamisi aliwaambia waandishi wa habari kwa kiburi na majivuno kuwa, "Tumepokea majibu kutoka kwa Waukraine ambao wamesema wanatumia kwa njia athirifu (silaha hizo)."
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani ameendelea kubwabwaja kwamba, wananchi wa Ukraine wanazitumia silaha hizo haramu kwa njia mwafaka kabisa, na kwamba anayetaka maelezo zaidi juu ya kadhia hiyo awasiliane na Ukraine.
Marekani imetuma nchini Ukraine silaha hizo zilizopigwa marufuku kimataifa, licha ya Rais wa Russia kuzitahadharisha nchi za Magharibi kuhusu kutuma mabomu hayo ya vishada huko Ukraine kwa kisingizio cha vita.
Rais Vladimir Putin wa Russia wiki iliyopita alijibu uamuzi huo wa Marekani kuhusu kutuma mabomu ya vishada huko Ukraine na kusema: Russia inaamini kuwa inayo haki ya kutoa jibu linaloshabihiana iwapo silaha hizo za vishada zitatumika dhidi ya nchi hiyo.
Kadhalika tangazo hilo la Marekani la kutuma mabomu ya vishada nchini Ukraine limepingwa pakubwa na kukabiliwa na radiamali mbalimbali kimataifa; kwani hata waitifaki wa Marekani ikiwemo Ujerumani, Uingereza, Canada na Uhispania pia zimetangaza waziwazi kwamba zinapinga uamuzi huo wa Washington.
Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Vishada ulianza kutekelezwa mwaka 2010, na tayari nchi zaidi ya 100 duniani zimesaini hati hiyo. Hata hivyo Marekani na Ukraine hazijasaini mkataba huo.