Jul 23, 2023 02:17 UTC
  • Taliban: Hatuhitaji kufanya mazungumzo wala kuwa na ushirikiano wowote na Marekani

Waziri wa Ulinzi wa serikali ya Taliban amekanusha madai ya kuwepo mtandao wa Al-Qaeda nchini Afghanistan na kusema, "sisi hatuhitaji kufanya mazungumzo yoyote au kuwa na ushirikiano wowote na Marekani.

Mullah Muhammad Yaqoub Mujahid, amepinga kuwa ushirikiano au kufanya mazungumzo yoyote na Marekani na kukanusha madai ya Magharibi kuhusu kuwepo kwa mtandao wa kigaidi Al-Qaeda nchini Afghanistan.
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Mullah Yaqoub amesema, Kabul haitamruhusu mtu yeyote kutumia ardhi ya Afghanistan ili kuhatarisha usalama wa nchi zingine na kwamba ripoti kuhusu kuwepo wanachama wa mtandao wa Al-Qaeda wanaohudumu kama washauri wa Taliban nchini Afghanistan ni "uongo".
 
Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Taliban amelitaja kundi la Daesh kuwa ni fitna dhidi ya Umma wa Kiislamu na akasema Taliban imetoa vipigo kadhaa kwa kundi hilo la kigaidi na kusisitiza pia kwamba, hakuna mwanamgambo yeyote wa kundi la Daesh katika safu za Taliban.

Bill Roggio, mhariri wa taasisi iitwayo The Foundation for the Defense of Democracies FDD, alidai siku ya Alhamisi kwamba kundi la Taliban linaisaidia na kuiunga mkono Al-Qaeda ndani ya Afghanistan na limewapa hifadhi wanachama wa kundi hilo. Roggio aliongeza kuwa Taliban imekuwa ikiunga mkono Al-Qaeda tangu Afghanistan ilipovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Marekani na kwamba hadi sasa inaendelea kufanya hivyo.

 
Utafiti unaofanywa na jopokazi la fikra la FDD, ambalo makao yake makuu yako mjini Washington, unajikita kwenye masuala ya usalama wa taifa na sera za nje za Marekani.../

Tags