Aug 16, 2023 02:48 UTC
  • Putin na Kim watilia mkazo kuwepo uhusiano wa karibu zaidi kati ya Russia na Korea Kaskazini

Rais Vladimir Putin wa Russia na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wameahidi kujenga ushirikiano wa karibu zaidi kati ya nchi zao mbili katika mawasiliano waliyofanya kwa barua kwa manasaba wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Ukombozi wa Korea Kaskazini.

Katika barua iliyotolewa na Kremlin ya ujumbe wa pongezi kwa Kiongozi wa Korea Kaskazini na wananchi wake, Putin amesema: "Nina hakika kwamba tutaendelea kujenga ushirikiano wa nchi mbili katika maeneo yote kwa manufaa ya watu wetu, kwa maslahi ya kuimarisha utulivu na usalama kwenye Peninsula ya Korea na katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Asia kwa ujumla".

Katika barua yake kwa Rais wa Russia kama ilivyoripotiwa na Shirika Kuu la Habari la Korea (KCNA), Kim amekumbusha jinsi urafiki wa nchi hizo mbili ulivyojengwa wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kwa ushindi dhidi ya Japan na akasema: "sasa inaonyesha kikamilifu jinsi Pyongyang na Moscow zisivyoshindika na zilivyo na uwezo mkubwa katika mapambano ya kuvunja ukiritimba na uasi wa mabeberu".

Aidha, Kiongozi wa Korea Kaskazini ameahidi kuendeleza uhusiano wa Moscow na Pyongyang ili uwe ni "uhusiano wa kimkakati wa muda mrefu."

Russia na Korea Kaskazini zimeimarisha zaidi uhusiano wao tangu vilipoanza vita nchini Ukraine Februari mwaka jana.

Kim amevielezea vita vya Ukraine kama "vita vya uwakala" vinavyopiganwa kwa niaba ya Marekani kwa lengo la kuiangamiza Russia. Amelaani pia msaada wa kijeshi wa nchi za Magharibi kwa Kiev na kukosoa alichokiita "sera ya ubabe na uamrishaji " na "uonevu" unaofanywa na Marekani na Magharibi katika mzozo huo.../

Tags