Sep 19, 2023 02:30 UTC
  • Kukata tamaa Marekani na Nato kuhusu ushindi wa Ukraine katika vita na Russia

Jenerali Mark Milley, mkuu wa majeshi ya Marekani, amesema ni vigumu kufikia natija ya haraka kuhusu vita vya Ukraine na kwamba muda mrefu zaidi unahitajika kabla ya Ukraine kufikia ushindi huo.

Hii ni katika hali ambayo tokea kuanza vita vya Ukraine na Russia, Rais Volodymyr Zelensky Ukraine amekuwa akipinga suala la kufanyika mazungumzo na Russia na kudai kuwa Moscow haina nia ya kufikia natija kuzungumza hayo. Rais huyo anaamini kuwa kuondoka askari jeshi wa Russia katika ardhi yote ya nchi hiyo ndio njia bora zaidi kuhusiana na suala hilo. Lakini mkuu wa majeshi ya Marekani, ambaye atastaafu mwishoni mwa Septemba, amesema kuwa jambo la kujiondoa kabisa Russia kutoka Ukraine, halitawezekana. Awali Milley alikuwa ametangaza kuwa subira inahitajika ili kufikia natija katika vita hivyo.

Milley anasema kuwa Russia ina zaidi ya askari jeshi elfu 200 nchini Ukraine. Hata kama majeshi ya Ukraine yatafikia malengo yake katika vita hivyo lakini kuondoa kikamilifu wanajeshi wa Russia katika ardhi ya nchi hiyo litakuwa jambo gumu mno.

Kuelezea mkuu huyo wa majeshi ya Marekani kutokuwa na imani kuhusiana na ushindi wa Ukraine katika vita vya sasa na Russia kuna kuja kwa kuzingatia kutofikia Kiev malengo yaliyotarajiwa katika mashambulizi yake mengi dhidi ya Russia katika maeneo ya  Mashariki  na Kusini Mashariki mwa nchi hiyo. White House inadai kuwa hadi sasa mapigano ya Ukraine yameigharimu zaidi ya dola bilioni 111 na hii ni licha ya Kyiv kupewa zana za kisasa na nchi za Magharibi. Vikosi vya nchi hiyo havijaweza kupata mafanikio ya kuzingatiwa katika mashambulizi dhidi ya Russia na vimeendelea kupata hasara tu. Seymour Hersh mwandishi wa habari maarufu wa Marekani, amemnukuu afisa mmoja wa kijasusi na kuripoti kwamba Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) lilimuarifu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken kwamba mashambulizi ya sasa ya  Ukraine dhidi ya Russia yameshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na kwamba hakuna matuamini ya kushindwa Russia  katika vita hivyo. Kwa hakika, kushindwa kufikia natija mashambulizi ya  Ukraine dhidi ya ngome za Russia mashariki mwa nchi hiyo, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakipewa umuhimu na vyombo vya habari na wanasiasa wa Magharibi yamewatia wasiwasi mkubwa waitifaki wake wa Magharibi. 

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg pia alionya katika mahojiano ya Jumapili kwamba vita vya Ukraine vinaweza kuwa vya muda mrefu, Kwa sababu mashambulizi ya nchi hiyo dhidi ya Russia hayajafikia natija za kuridhisha. Ameonya kuwa nchi za Magharibi zinapasa kujiandaa kwa ajili ya vita vya muda mrefu nchini Ukraine.

Zana za Kimarekani nchini Ukraine

 

Hii ni katika hali ambayo Russia pamoja na  kusisitiza juu ya kutokuwa na natija mashambulizi ya Ukraine dhidi yake imetangaza kuwa jeshi la Kiev limepata hasara kubwa ya kibinadamu na kupoteza zana zake nyingi. Kwa mujibu wa Rais Vladmir Putin wa Russia, serikali ya Kiev imepoteza zaidi ya askari elfu 71 tokea kuanza operesheni yake ya kujibu mashambulizi ya Russia mwezi Juni. Kwa mujibu wa vyanzo vya Kiukreni, vitengo vingine vimepoteza asilimia 90 ya wafanyakazi wake. 

Licha ya ukweli huo lakini Marekani na Nato bado zinataka kuendeleza vita vya umwagaji damu huko Ukraine. Stoltenberg amesisitiza kuhusiana na suala hilo kwamba NATO itaendeleza jitihada zake za kijeshi na si za kidiplomasia. Katibu Mkuu huyo wa Nato ameongeza kuhusiana na jambo hilo kuwa wanapasa kukubali kwamba ikiwa Zelensky na Waukraine watasimamisha vita, nchi yao haitakuwepo tena,  na kuwa amani itapatikana tu pale Putin na jeshi lake watakapokubali kuweka chini silaha zao.

Wakuu wa Marekani na NATO wanaamini kwamba ushindi wa Russia katika vita vya Ukraine, vinavyoendelea kwa uungaji mkono wa NATO, utapelekea kukosa itibari shirika hilo la kijeshi na kuongezeka ushawishi na uwezo wa Moscow kieneo na kimataifa hatua ambayo itabadilisha uwiano wa kiusalama na kijeshi katika nchi za Ulaya. Ni kwa sababu hiyo ndiyo Marekani na waitifaki wake wa Ulaya wakatoa kipaumbele kwa ajenda ya kupelekwa nchini Ukraine  kila aina ya silaha  za masafa marefu kama vile makombora ya Himars na Atakams pamoja na aina  nyingine ya silaha  nzito. Hata hivyo, hatua hizo zimeongeza tu muda wa vita hivyo visivyo na natija kwa Ukraine na kuifanya serikali ya Kiev iendelee kutozingatia masuala ya amani nchini humo. 

 

Tags