Sep 30, 2023 15:46 UTC

Mwanazuoni wa madhehebu ya Suni nchini Ghana amesema kuwa, umoja wa Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, unastahiki sifa na ni nembo ya mshikamano wa Waislamu.

Sheikh Mohammed Kashif Asrar, ambaye ni miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kisuni na kiongozi wa kundi la Kiislamu la Wataniyah la Ghana, amezungumzia umuhimu wa umoja wa Kiislamu kwa kuzingatia njama zinazofanywa dhidi ya Waislamu, na kusema kwamba, Waislamu wanapaswa kushirikiana ndani ya mfumo wa lengo moja katika Quran Tukufu.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu wa Ghana ameongeza kuwa: Waislamu wanakuwa imana na wenye nguvu kubwa kutokana na umoja; na katika hali kama hiyo, wanaweza kupambana na maadui.

Mohammed Kashif Asrar amesema kuwa, Waislamu wana mambo yanayowakutanisha pamoja kama Mtume Muhammad (SAW), Qur'ani Tukufu na Kibla kimoja, na mambo hayo yanatosha kuimarisha mafungamano na umoja; hivyo Waislamu wanapaswa kuwa Umma mmoja bila kujali madhehebu na makundi yao.

Vilevile ameashiria kadhia ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Ulaya na kusema, umoja wa Kiislamu una nafasi muhimu katika kufuatilia hatua za kisheria katika uga wa kimataifa kwa shabaha ya kuzuia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Mohammed Kashif Asrar amefafanua kwamba, leo Uislamu unakabiliwa na adui katika nchi za Magharibi na kwamba kuchomwa moto nakala za Qurani, kuharibu misikiti na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (SAW) ni mifano ya uadui huo.

Amepongeza msimamo wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuhusu suala la kuvunjiwa heshima Qur'ani tukufu katika nchi za ulaya na kuyahimiza makundi yote ya Kiislamu kuitikia wito wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran wa kukabiliana na suala hilo. 

Tags