Oct 06, 2023 10:36 UTC
  • Putin: Ndege iliyombeba kiongozi wa Wagner iliripuka kwa maguruneti yaliyokuwemo ndani yake

Rais Vladimir Putin wa Russia amedokeza kuwa ajali ya ndege iliyomuua mkuu wa kikosi cha mamluki cha Wagner, Yevgeny Prigozhin ilisababishwa na mripuko wa maguruneti yaliyokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Kwa mujibu wa Putin, ndege ya Prigozhin iliripuliwa kutokea ndani, na si kwa kupigwa kombora kama ilivyokuwa imevumishwa, akibainisha kuwa mkuu wa kamati ya uchunguzi ya Russia ameripoti kwamba athari za mada za miripuko ziligunduliwa katika miili ya waliofariki katika ajali hiyo mnamo mwezi Agosti.

"Hakukuwa na athari za kutokea nje ya ndege, huu tayari ni ukweli uliothibitishwa," ameeleza rais wa Russia, akionekana kutupilia mbali madai ya maafisa wa Merika ambao waliamini kuwa ndege iliyokuwa imembeba kiongozi wa kundi la Wagner ilitunguliwa.

Putin (kushoto) na Prigozhin

Ndege ya binafsi ya Embraer ambayo Prigozhin alikuwa akisafiria kwenda Saint Petersburg ilianguka kaskazini mwa Moscow na kuua watu wote 10 waliokuwemo ndani yake mnamo Agosti 23. Watu wengine wawili ambao ni viongozi waandamizi wa Wagner, pamoja na walinzi wanne wa Prigozhin na wafanyakazi watatu ni miongoni mwa waliouawa.

Prigozhin alikufa katika ajali hiyo miezi miwili baada ya kuongoza uasi wa muda mfupi dhidi ya mamlaka za ulinzi za Russia na kutoa changamoto kubwa kwa utawala wa Putin tangu aingie madarakani mwaka 1999.

Kikosi cha mamluki cha kundi la Wagner ambacho kiliasisiwa na Prigozhin kilikuwa kikifanya kazi nchini Ukraine, Syria, Libya na nchi nyingine kadhaa za Afrika na kilifikia kuwa na idadi ya makumi ya maelfu ya wapiganaji katika kilele cha harakati zake.

Kwa mujibu wa Rais wa Russia, wapiganaji elfu kadhaa wa kundi hilo tayari wameshasaini mikataba ya utiifu na vikosi vya jeshi la nchi hiyo.../

Tags