Vladimir Putin: Wakati umefika wa kutangazwa nchi huru ya Palestina
Rais Vladimir Putin wa Russia amezungumzia kushindwa siasa za kibeberu za rais wa Marekani, Joe Biden za kuingilia masuala ya eneo la Asia Magharibi na kutilia mkazo wajibu wa kutekelezwa maamizio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayosisitizia kuundwa nchi huru ya Palestina.
Rais Putin alisema hayo jana Jumanne kabla ya kuanza mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Iraq, Muhammad Shia al Sudani na kuongeza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa Palestina ni kutekelezwa maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kutangazwa nchi huru ya Palestina.
Matamshi hayo ya Rais wa Russia yamekuja huku wanamapambano wa Palestina wakiendelea na mapambano yao ya kishujaa ya kukabiliana na wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vitongoji kadhaa vya karibu na Ukanda wa Ghaza.
 
Mujahidina wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wameendelea kuvitwanga kwa makombora vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vikiwemo vya Asqalan na Ashdod pamoja na Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya mji wa Baytul Muqaddas; yakiwa ni majibu kwa jinai za utawala wa Kizayuni za kuua kikatili watoto, wanawake na wananchi wa kawaida wa Palestina.
Operesheni ya kishujaa na ya kihistoria ya Kimbunga cha al Aqsa ilianza siku ya Jumamosi wiki hii kwa wanamapambano wa Palestina kuwashtukiza Wazayuni kwa kuteka kambi zao za kijeshi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni pamoja na kuangamiza mamia ya wanajeshi wa Israel na kuteka nyara Wazayuni wasio na idadi.
Hadi tunaripoti habari hii, zaidi ya Wazayuni 1,200 walikuwa wameshaangamizwa na zaidi ya 2000 wengine wameshajeruhiwa na idadi isiyojulikana wako mikononi mwa wanamapambano wa Palestina tangu ilipoanza operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa siku ya Jumamosi.
 
							 
						 
						