Oct 28, 2023 02:22 UTC
  • Radiamali ya China kuhusu ripoti ya mwaka ya Pentagon

Wizara ya Ulinzi ya China imelaani ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kuhusu nchi hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesisitiza katika ripoti hiyo kwamba China katika miaka kumi ijayo itajiimarisha kijeshi kwa kuzifanya za kisasa zana zake za nyuklia. Pentagon imedai kuwa China ina zaidi ya vichwa 500 vya nyuklia na huenda kufikia 2030 vitakuwa vimefikia zaidi ya vichwa elfu moja. Hii ni katika hali ambayo, Beijing inapinga madai hayo na inaamini kuwa Marekani inajaribu kuhalalisha sera zake za kijeshi Asia Mashariki kwa kueneza propaganda na siasa chafu dhidi yake.

Lee T-Wan, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo kuwa Marekani inafuatilia malengo mawili kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi na za uwongo dhidi ya maadui na wapinzani wake. La kwanza inajaribu kuhalalisha ongezeko la bajeti yake ya kijeshi ambayo hufanyika kila mwaka na pili ni kuhalalisha vikwazo vyake dhidi ya China kwa kujaribu kuionyesha kuwa ni adui wake wa kwanza.

Katika barua yake kwa Kamati ya Kitaifa ya Mahusiano ya Marekani na China yenye makao yake huko New York, Rais Xi Jinping wa China alisema kwamba Beijing iko tayari kuwa na ushirikiano na Marekani utakaoziridhisha pande zote.

Pentagon

Alisisitiza kuwa China na Marekani zikiwa nchi mbili kubwa duniani, zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha amani ya dunia na mustakabali wa binadamu kwa kuchagua njia sahihi na kuwa na maingiliano mazuri kati ya serikali mbili. Hii ni katika hali ambayo Marekani daima imekuwa ikipinga na kulifanyia dharau ombi hilo la China la kuwepo ushirikiano wa pande mbili kwa manufaa ya mataifa mawili.

Beijing inasisitiza kuwa iko tayari kushirikiana na Washington ili kukuza ushirikiano kwa manufaa ya pande zote, kutatua tofauti, kukabiliana na changamoto za kimataifa na kusaidia kuimarika kila mmoja chini ya misingi ya kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kuboresha ushirikiano wa pande mbili. Siasa ambazo si tu kwamba Marekani haizikubali, bali pia inajaribu kuilazimisha China ifuate siasa na mipango ya Washington.

China inaamini kwamba siasa hizo za Washington zimepitwa na wakati katika mazingira ya hivi sasa ya kimataifa na kuwa nchi hiyo inapaswa kuwasilisha kimataifa mipango na sera mpya zitakazoboresha ushirikiano sahihi wa kimataifa

Abolfazl Zahrawand, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusu hili: Marekani ina wasiwasi wa kupoteza satwa yake ya kimataifa kwa China na mataifa mengine yenye nguvu kikanda na kimataifa. Ni kwa sababu hiyo ndio imeegemeza siasa zake zote katika kuidhoofisha China, na wala haina nia ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na Beijing. Baadhi ya mirengo ya Marekani hata inaamini kuwa kushirikiana na China kutapelekea kuimarika zaidi nguvu zake za kimataifa.

Kwa vyovyote vile, uingiliaji wa hivi karibuni wa Marekani katika suala la kugongana meli za China na Ufilipino unaonyesha kuwa Washington inatumia kila  fursa kwa ajili ya kuibua mgogoro dhidi ya China.

Kuhusu suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesisitiza kuwa suala la kugongana meli za nchi hiyo na Ufilipino katika eneo linalozozaniwa ni suala linalozihusu Beijing na Manila pekee na wala halihitajii uingiliaji wa Marekani.

Mao Ning

Kwa mujibu wa Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, kisiwa cha Thams Shoal kijiografia, kiuchumi, kisiasa na kihistoria ni sehemu muhimu ya Visiwa vya Spartan vya Bahari ya Kusini ya China kwa mujibu sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Hati ya Umoja wa Mataifa. Kwa maneno yake, Beijing inaiona hukumu iliyotolewa na mahakama ya usuluhishi wa Bahari ya Kusini ya China kuwa batili na inaamini kuwa, hatua ya Marekani ya kutumia vibaya hukumu hiyo haramu haitakuwa na taathira yoyote kwa azma ya Beijing ya kulinda mamlaka yake ya ardhi, kisheria pamoja na maslahi ya baharini katika eneo hilo. Hii inaonyesha kuwa suala la ardhi ni mstari mwekundu kwa China na kamwe haitaruhusu Marekani kuibua mgogoro katika eneo kwa kuingilia masuala yanayohusu ardhi ya China. Kwa hiyo, inaonekana kwamba idara mbalimbali za kijeshi na kiusalama za Marekani zinatekeleza wazi wazi siasa za pamoja za kuharibu usalama na jina la China.

 

Tags