Nov 10, 2023 02:52 UTC
  • Utunishaji misuli wa China sambamba na harakati za Marekani katika Bahari ya China Kusini

China imetuma meli yake ya kivita ya kubeba ndege ya Shangong katika Bahari ya China Kusini sambamba na kufanyika maneva ya baharini kati ya Marekani, Korea Kusini na Ufilipino.

Hii ni mara ya tatu kwa China kutuma manowari yake hiyo ya Shandong huko magharibi mwa Bahari ya Pacific. Marekani siku zote imekuwa ikifanya maneva za kijeshi na Korea Kusini na Japan, na kwa msingi huo, ni jambo la kushangaza na kuzingatiwa kuhusu lengo hasa la Marekani kuishirikisha Ufilipino katika maneva ya sasa badala ya Japan. Awali ni kuwa, Ufilipino na China zina hitilafu za mpaka na ardhi katika Bahari ya China Kusini, na Marekani inataka kunufaika na hitilafu hizo ili kuendelea kuyumbisha hali ya usalama ya eneo hilo. 

Pili ni kuwa, Ufilipino ni kituo muhimu cha Marekani huko kusini mashariki mwa bara la Asia; na kushiriki nchi hiyo katika maneva hiyo tajwa ni ishara ya kuboreka nafasi ya kijeshi ya Marekani katika eneo. Hii ni kwa sababu, wakati wa  utawala wa Rais Duterte huko Ufilipino, uhusiano kati ya nchi hiyo na Marekani ulikuwa baridi kwa kiasi fulani kutokana na sera ya rais huyo ya kuweka mlingano kati ya Beijing na Washington. Kwa msingi huo, kushiriki jeshi la Uflipino katika maneva na Marekani ni dhihirisho la nguvu la nchi hiyo mkabala wa China, hatua inayodhirisha kujiunga Ufilipino na kambi ya Marekani. 

Rais mstaafu wa Ufilipino, Rodrigo Duterte 

Lee Haidong mchambuzi wa masuala ya kisiasa anazungumzia suala hilo kwa kusema: "Ingawa msimamo wa Japan na Korea Kusini uko wazi kikamilifu kuhusu sera za Marekani katika eneo lakini inaonekana kuwa sifa pekee na umuhimu wa maneva hayo ya sasa ni ushiriki wa Ufilipino katika mazoezi hayo ya kijeshi."  

Hakuna shaka kuwa nguvu za kijeshi za nchi hii haziwezi kulinganishwa na China kwa namna yoyote ile, hata hivyo Marekani kwa kuendesha maneva ya kijeshi ya pamoja na nchi zilizo na  hitilafu za ardhi  na mipaka na China inajaribu kuonyesha nguvu zake mkabala wa Beijing ambayo imefanikiwa kuwa na taathira katika eneo. 

Hata kama inasemekana kuwa mazoezi hayo ya kijeshi kati ya vikosi vya majini vya Marekani vya Reagan na Vinson CSG na jeshi la wanamaji la Japan yalianza Jumamosi iliyopita na yangali yanaendelea; lakini China inatambua vyema aina ya ushirikiano na ushiriki wa Marekani katika maneva hiyo, na inaamini kuwa upo uwezekano mdogo sana wa kujiri vita kati yake na Japan. Hii ni kwa sababu, Japan inafahamu vyema kwamba iwapo vita vitatokea, uchumi wa nchi hiyo unaotegemea mauzo ya nje utasambaratika. Wakati huo huo China inatilia maanani ushiriki wa Ufilipino katika maneva ya Marekani na kuamini kuwa ni kitendo chenye taathira hatari; kwa sababu huenda serikali ya Manila ikakabiliwa na mashinikizo ya Marekani, kuchochewa au kushawishiwa na misaada ya kifedha na kijeshi ya Marekani kupitia hitilafu hizo za ardhi na mipaka na hivyo kuchukua hatua ambayo haitakuwa na maslahi yoyote kwa eneo. Ndio maana Msemaji wa Kamandi ya Kusini ya jeshi la China hivi karibuni akaitahadharisha Ufilipino akisema nchi hiyo inapasa kusitisha mara moja hatua zake za uchochezi na kujiepusha na kushadidisha mivutano. 

Maneva ya China

Lee Ming mchambuzi wa masuala ya kimataifa anazungumzia kadhia hii akisema: "Ufilipino ndiyo kiungo dhaifu zaidi cha kijeshi cha Marekani huko kusini mashariki mwa Asia; na Washington haifanyi lolote kuimarisha nafasi ya kiuchumi na kijeshi ya Ufilipino licha ya kuasisi vituo vyake vya kijeshi nchini humo bali nchi hiyo inahesabiwa kuwa ardhi na pepo ya wanajeshi wa Marekani. Kwa msingi huo, Beijing inauzingatia pakubwa uwezekano wa serikali ya Manila kuchukua hatua haribifu dhidi ya China kwa kushawishiwa na kuchochewa na Marekani. 

Ala Kulli haal, kwa kuzingatia kuwa katika miezi ya karibuni kumepamba moto hitilafu kati ya China na Ufilipino kuhusu baadhi ya visiwa na maeneo ya mipaka katika Bahari ya China Kusini; kushiriki Ufilipino katika maneva ya Marekani na Japan kutazidisha hisia tofauti; na wakati huo huo kuitia wasiwasi China. Hasa ikizingatiwa kuwa Waziri Mkuu wa Japan pia  tarehe 3 mwezi huu wa Novemba alielekea Manila kwa ajili ya ziara ya siku mbili ambapo lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya Tokyo, Manila na Washington kwa ajili ya kile kinachotajwa kuwa "Kukabiliana na Vitisho vya China." Ni kwa sababu hii ndio maana China nayo imeamua kupelekea meli zake za kijeshi katika Bahari ya China Kusini ili kuonyesha kuwa iko tayari kikamilifu kukabiliana na hatua zozote za uharibifu za Marekani na washirika wake dhidi yake.

Tags