Sisitizo la Putin la kutoziami nchi za Magharibi
(last modified Tue, 19 Dec 2023 02:34:22 GMT )
Dec 19, 2023 02:34 UTC
  • Vladimir Putin
    Vladimir Putin

Siku ya Jumapili, Rais Vladimir Putin wa Russia alikiri katika hotuba isiyokuwa ya kawaida kwamba ni makosa kuzidhania vizuri na kuzitegemea nchi za Magharibi na kufikiria kuwa Russia haina tofauti na nchi hizo. Alisema: Nilidhani kimakosa kuwa hakungekuwepo mzozo kati ya Russia na nchi za Magharibi na kwamba ulimwengu ulikuwa umebadilika.

Putin alisema katika miaka ya kwanza ya muongo wa 2000, alikuwa akidhani kwamba ulimwengu ulikuwa umebadilika na kwamba hakungeshuhudiwa makabiliano ya kiitikadi wala sababu za kutokea migogoro kati ya nchi za Magharibi na Russia. Alisema: 'Nilifikiria kiuanagenzi kwamba ulimwengu wote, hasa ulimwengu unaodaiwa kuwa umestaarabika wa Magharibi, ulielewa vizuri kile kilichotokea Russia, kwamba imekuwa nchi tofauti kabisa, kuwa kile kilichotokea kimepelekea kutokuwepo mzozo wa kiitikadi na kwamba hakuna tena sababu ya kuwepo makabiliano.'

Kukiri huko kwa Rais wa Russia kuhusiana na kutoaminika nchi za Magharibi kunatokana na siasa za uhasama ambazo zimekuwa zikitekelezwa na nchi hizo dhidi ya Moscow katika miongo kadhaa iliyopita, baada ya kumalizika kipindi cha Vita Baridi. Russia, ikiwa mrithi wa Umoja wa Sovieti ya zamani na katika miaka ya 1990 wakati wa uongozi wa Boris Yeltsin, ilikuwa na mtazamo chanya kuhusiana na nchi za Magharibi, na hata viongozi wakuu wa nchi hiyo wakidhani kwamba wangeweza kujiunga na taasisi za Magharibi na Ulaya. Hata hivyo, mtazamo huo ulianza kubadilika taratibu kutokana na hatua za uhasama za nchi za Magharibi dhidi ya Russia, hususan juhudi za NATO za kujitanua upande wa Mashariki na kuzijumuisha nchi za Ulaya Mashariki na Kati ambazo hapo awali zilikuwa wanachama wa Mkataba wa Warsaw. Katika hatua iliyofuata, NATO, ikiongozwa na Marekani, ilifanya jaribio la wazi la kuzifanya nchi zilizo karibu na Russia, hasa Ukraine na Georgia, kuwa wanachama wa shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi, hatua ambayo ilimaanisha kujaribu kuidhibiti Russia, na hilo likachochea hisia kali za Moscow.

Nato

Kwa kweli, chanzo cha vita viwili, yaani, vita kati ya Russia na Georgia mwaka 2008 na kati ya Russia na Ukraine kuanzia Februari 2022 hadi sasa, kinatokana na suala hilo hilo. Mtazamo wa uhasama wa NATO na kuendelea na juhudi zake za kusonga mbele kuelekea Mashariki kumeifanya Russia kuiona NATO kuwa tishio kubwa kwa usalama wake. Kwa mtazamo wa viongozi wa Kremlin, uadui na uhasama wa Wamagharibi dhidi ya Russia si jambo la muda tu, bali ni sera endelevu na thabiti ambayo inatekelezwa na NATO na Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Viongozi wa Moscow wamefikia natija kwamba uadui wa Wamagharibi dhidi ya Russia si jambo la muda tu, bali ni siasa endelevu za NATO na Marekani kwa ajili ya kuidhibiti Russia. Katika uwanja huo, Wamagharibi si tu kwamba wanatishia usalama wa taifa la Russia, bali daima wanawaunga mkono wapinzani wa serikali ya Moscow na wale wanaotaka kujitenga na nchi hiyo na hivyo kuingilia moja kwa moja mambo ya ndani ya nchi hiyo. Katika muktadha huo, Putin amesema: 'Ninaamini mia kwa mia kwamba baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti ya zamani nchi za Magharibi zilidhani kwamba Russia nayo hatimaye ingesambaratika tu na kuwa walichopasa kufanya ni kuwa na subira hadi jambo hilo litimiye.'

Kwa upande mwingine, Russia, ikiwa nchi pekee iliyo na nguvu sawa za nyuklia na Marekani, daima imekuwa ikitazamwa na nchi hiyo ya Magharibi kuwa tishio kubwa kwake kiusalama na ndio maana Washington ikatumia uwezo wake wote kwa ajili ya kutaka kuitenga na kuidhoofisha kimataifa. Kwa mtazamo wa Washington, vita vya Ukraine vimetoa fursa nzuri kwa ajili ya kudhoofishwa Russia na Putin na hatimaye kumpelekea aondoke madarakani. Marekani daima imekuwa ikiitaja Russia kama mshindani na tishio katika nyaraka zake za kiusalama na za siri. Sababu ya Washington kuchukua msimamo huo ni hatua ya Moscow ya kutaka mabadiliko yafanyike katika mfumo wa uongozi wa dunia kwa kutilia maaani mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yametokea ulimwenguni, na pia kutolewa fursa kwa Umoja wa Mataifa ili uweze kuwa na mchango zaidi katika kushughulikia utatuzi wa mizozo ya kieneo na kimataifa.