Jan 14, 2024 03:32 UTC
  • Walimwengu waandamana kulaani siku 100 za jinai za Israel Gaza

Mamilioni ya watu jana Jumamosi walifanya maandamano katika pembe mbali mbali za dunia kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na vile vile kuonyesha mshikamano wao na taifa la Palestina.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, mamilioni ya watu katika miji na majiji 121 kwenye nchi 45 kote duniani walijitokeza mabarabarani kushiriki maandamano hayo ya kulaani siku 100 za jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza, chini ya kaulimbiu ya "Siku ya Hatua ya Ulimwengu."

Walimwengu walioshiriki kwa wingi maandamano hayo ya jana walitoa wito wa kusitishwa mara moja vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Katika maandamano hayo, wananchi katika nchi za Kiislamu walichoma moto bendera za Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel na kutangaza mshikamano wao na wananchi wa Palestina, sanjari na kutaka kusitishwa vita huko Gaza.

Waandamanaji nchini Afrika Kusini katika miji ya Cape Town na Johannesburg mbali na kutangaza mshikamano na taifa madhulumu la Palestina, walitumia maandamano hayo kuunga mkono na kupongeza hatua ya serikali yao ya kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya Israel, kutokana na jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza.

Aidha maelfu ya watu nchini Nigeria walishiriki kwenye maandamano yaliyofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Abuja kulaani siku 100 za jinai za Israel huko Gaza, yaliyoandaliwa na Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Kadhalika waungaji mkono wa wananchi madhulumu wa Palestina nchini Marekani jana walikusanyika mbele ya Ikulu ya White House mjini Washington wakipinga siasa za serikali ya nchi yao za kutoa himaya kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Halikadhalika jana Jumamosi mamilioni ya watu katika nchi za Ulaya walijitokeza kwa wingi barabarani katika miji mbalimbali kuanzia London, Paris, Sydney, hadi Tokyo Japan, na kueleza mshikamano wao na watu wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza.

Mamilioni ya Wayemen katika maandamano ya kuunga mkono Palestina, muqawama

Utawala katili wa Israel umekuwa ukishambulia na kulipua kwa mabomu eneo hilo linalozingirwa kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, ili kulipiza kisasi cha shambulizi la kushtukiza la Kimbunga cha al-Aqsa la Oktoba 7 mwaka jana.

Tangu yalipoanza mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, Wapalestina karibu 24,000, aghalabu yao wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 60,000 kujeruhiwa.

Tags