Russia: Amani ya Ukraine inategemea kusimamishwa upelekekaji silaha nchini humo
(last modified Mon, 15 Jan 2024 13:59:45 GMT )
Jan 15, 2024 13:59 UTC
  • Maria Zakharova
    Maria Zakharova

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa mazungumzo ya amani kwa ajili ya Ukraine yanawezeka tu kwa kusimamishwa upelekaji wa silaha kwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Farsi limemnukuu Maria Zakharova akisema kuwa, nchi za Magharibi zinapasa kuacha kuipatia Kyiv silaha kama zinataka mazungumzo ya amani kwa ajili ya Ukraine. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameeleza haya akijibu matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswisi aliyezungumzia suala la kushiriki Moscow katika mchakato wa amani ya Ukraine.  

Wakati huo huo Zakharova ametahadharisha kuwa Moscow haitafanya mazungumzo na upande wowote iwapo madhumuni ya matamshi ya baadhi ya nchi za Magharibi ni kuiingiza Russia katika mchakato wa uwongo kwa kuzingatia masharti ya nchi za Magharibi ili kuathiri misingi ya sheria za Russia. 

Itakumbukwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswisi, Ignazio Cassis, alisema jana Jumapili, kando ya mkutano wa amani kuhusu Ukraine uliofanyika katika mji wa Davos kwamba, nchi kadhaa zinafuatilia suala la upatanishi ili Russia ishiriki katika mazungumzo ya amani ya Ukraine. 

Annalena Baerbock (kulia( na Stéphane Séjourné, 
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani na Ufaransa

Annalena Baerbock Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani  pia amesema kuwa ipo haja kuendeleza misaada ya Ulaya kwa Ukraine madhali Russia bado haijatoka katika ardhi ya Ukraine. 

Russia imekuwa ikisema mara kwa mara kuwa hatua ya nchi za Magharibi ya kutuma silaha Ukraine itarefusha mzozo nchini humo na matukio yasiyotabirika.