Kesi iliyofunguliwa na A/Kusini dhidi ya Israel yaendelea kuungwa mkono
(last modified Mon, 22 Jan 2024 02:58:16 GMT )
Jan 22, 2024 02:58 UTC
  • Kesi iliyofunguliwa na A/Kusini dhidi ya Israel yaendelea kuungwa mkono

Kwa mara nyingine tena, Ubelgiji imejiunga kwenye safu ndefu ya waungaji mkono wa hatua ya Afrika ya Kusini ya kufungua kesi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kutokana na jinai zake za kupindukia dhidi ya watoto wachanga, wanawake, vizee na watu wa kawaida huko Ghaza.

Kesi ya kihistoria iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala katili wa Kizayuni imewafurahisha walimwengu katika kona zote za dunia.

Katika siku za awali tu za mwaka mpya wa 2024, Afrika Kusini iliushitaki utawala wa Kizayuni kwa kufanya mauaji ya kimbari na kukanyaga sheria za kimataifa tangu mwaka 1948 hadi hivi sasa.

Mahakama ya Kimataifa ya ICJ ilisikiliza kesi hiyo tarehe 11 na 12 za mwezi huu wa Januari na hiyo ilikuwa ni hatua ya kihistoria ya kuburuzwa kizimbani utawala wa Kizayuni kutokana na mauji yake ya kizazi cha Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza,

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Bi Caroline Gennez, Waziri wa Misaada ya Ujenzi na Ustawi wa Ubelgiji amegusia suala la kusikilizwa kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel inayofanya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Ghaza na kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba iwapo Mahakama ya Kimataifa ya ICJ itatoa hukumu dhidi ya Israel katika kesi hiyo, Ubelgiji itaiunga mkono kikamilifu hukumu hiyo.

Kabla ya hapo pia Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji sambamba na kulaani jinai za Israel kwenye Ukanda wa Ghaza naye alitangaza kuunga mkono kikamilifu hatua ya Afrika Kusini ya kuishitaki Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICJ kutokana na jinai zake kubwa mno dhidi ya wananchi wa Ghaza.

Nchi nyingi duniani pamoja na wataalamu zaidi ya 200 na maprofesa wa sheria za kimataifa nao wametangaza waziwazi kuwa wanaunga mkono hatua hiyo ya Afrika Kusini kama ambavyo wanaunga mkono pia kutolewa hukumu dhidi ya utawala wa Kizayuni katika mahakama hiyo.