Feb 03, 2024 08:48 UTC
  • Algeria yawasilisha muswada wa azimio la kusitishwa vita huko Gaza

Algeria imetoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza katika rasimu ya azimio iliyowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rasimu hiyo iliyotayarishwa na Algeria inapinga suala la Wapalestina kulazimishwa kuhama makazi yao, na kwa mara nyingine tena inasisitiza ulazima wa pande mbili kuheshimu sheria za kimataifa.

Rasimu hiyo pia inataka kufikishwa kikamilifu, haraka, salama na bila ya kizuizi misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Rasimu hiyo iliyowasilishwa na Algeria katika Baraza la Usalama la UN inahitaji kura zisizopungua 9 za wanachama 15 wa baraza hilo.

Mwezi Disemba mwaka jana, Baraza la Usalama lilipitisha azimio la kudhamini ongezeko la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza, lakini baada ya kucheleweshwa upigaji kura kwa wiki moja na mazungumzo ya kuzuia Marekani kutumia kura ya veto, azimio lililopasishwa halikutoa wito wa kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, Wapalestina zaidi ya elfu 27 wameuawa shahidi hadi sasa katika mashambulizi ya kikatili ya Israel wengine zaidi ya elfu 66 wamejeruhiwa.

Tags