IHRC yaitaka jamii ya kimataifa kukomesha mateso ya Waislamu wa Myanmar
Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu yenye makao yake London nchini Uingereza (IHRC) imesema kuwa kutokuwepo mashinikizo ya kimataifa ndiyo sababu ya kuendelea mateso na ukandamiza wa mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.
Mwananchama wa kamisheni hiyo, Arzu Merali amesema ukosoaji hafifu wa jumuiya za kimataifa kuhusu dhulma wanazofanyiwa Waislamu wa Myanmar hauna taathira yoyote na kwamba kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu ukatili unaofanywa dhidi ya Waislamu wa Myanmar ni miongoni mwa sababu kuu za mgogoro huo.
Merali amesema kuwa, jamii ya kimataifa haijachukua hatua yoyote ya kivitendo ya kuishinikiza serikali ya Myanmar na kwa msingi huo watawala wa nchi hiyo hawaoni sababu ya kubadili sera na siasa zao kuhusu jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.
Mwanachama huyo wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu amesema kuwa, madola makubwa hususan Marekani yanafuatilia maslahi yao na kwamba yamenyamazia kimya mauaji na mateso ya Waislamu wa Myanmar kwa sababu hayagusi maslahi ya nchi hizo.
Maelfu ya Waislamu wa Myanmar wameuawa na malaki ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na madhudha wenye misimamo mikali dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya.