Ripoti ya UN: Israel inawatesa vikali wafungwa Wapalestina
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imewatuhumu wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuwatesa kinyama raia Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, wakiwemo wanawake na wanaume. Wapalestina hao walioteshwa vikali ni wale waliotekwa katika vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza.
Ripoti hiyo imetayarishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), ambapo imebainisha kuwa mamia ya watu wa Gaza wamekuwa wakiteshwa vikali katika vizuizi vya utawala wa Kizayuni wa Israel tokea Oktoba mwaka jana wakati utawala wa Kizayuni wa Israeli ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari Gaza.
Ripoti hiyo imebaini kuwa takriban wafungwa 1,000 wanashikiliwa bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote katika maeneo matatu ya kijeshi ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na kuongeza kuwa baadhi yao wamefariki wakiwa kizuizini.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Palestina lilisema Jumatatu kwamba baada ya kuachiliwa, wafungwa wa Gaza walirudi "wakiwa na kiwewe kabisa," wakiripoti dhulma kubwa walizotendewa kizuizini.
Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini amekiambia kikao cha wanahabari kwamba wafungwa Wapalestina wamekuwa wakikabiliwa na kiwango kikubwa cha udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kupewa pigo la umeme, kupigwa picha wakiwa uchi, kunyimwa usingizi na kuwekwa karibu na mbwa wa kuwatisha,
Timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa pia imesema kwamba wamepokea taarifa kutoka vyanzo vya taasisi na mashirika ya kiraia na mahojiano ya moja kwa moja, kuhusu "unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanaume na wanawake wa Palestina katika vizuizi vya utawala wa Israel, wakati wa uvamizi wa nyumba na katika vituo vya ukaguzi."
Mwanamke mwenye umri wa miaka 39 kutoka Gaza City, ambaye utambulisho wake haujafichuliwa amesema, "Askari walikuwa wakali sana, walitupiga na kutuzomea kwa Kiebrania."
Mwezi uliopita, kundi la wataalamu walioteuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilitoa hofu kuhusu ukiukwaji wa haki dhidi ya wanawake na wasichana wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wakati huo huo, UNRWA pia imekosoa utawala wa Israel kwa kuwatendea vibaya "wafanyakazi wake kadhaa kutoka Ukanda wa Gaza," ambao walizuiliwa na vikosi vya Israel na kudhulumiwa wakiwa kizuizini.