Russia: Nchi za Magharibi zinacheza na moto katika ardhi ya Ukraine
Serikali ya Russia imetoa onyo kali kwa madola ya Magharibi na kusema kuwa, baadhi ya mataifa ya Magharibi yanacheza na moto kwa kujadili wazo la kutuma wanajeshi wao nchini Ukraine.
Onyo hilo limetolewa na Dmitry Peskov, Msemaji wa Ikulu ya Russia, Kremlin na kuongeza kuwa, matamshi ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kuhusu jambo hilo yamepokewa kwa hisia kali na Moscow.
Paskov amesema: "Rais wa Ufaransa anajadili wazo la kutuma kikosi cha kigeni. Wote wanacheza na moto. Hii ni tabia ya kutowajibika sana kwa wanasiasa."
Hivi karibuni Macron alisema kwamba, suala la uwezekano wa kutumwa wanajeshi wa kigeni nchini Ukraine lilijadiliwa wakati wa mkutano wa mjini Paris. Alisema ingawa hakukuwa na makubaliano rasmi kati ya viongozi wa Ulaya lakini jambo hilo halipaswi kupuuzwa.
Pia alisema muungano mpya utaanzishwa ili kuipa Kiev silaha za masafa ya kati na marefu. Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa vikosi maalumu vya nchi za Magharibi tayari viko Ukraine licha ya suala hilo kukanushwa NATO.
Rais Vladimir Putin wa Russia ametoa onyo kali akisema kuwa, kutumwa wanajeshi wa nchi za Magharibi kwenda kupigana nchini Ukraine kuna hatari ya kuzusha vita vya nyuklia duniani.
Katika matamshi yake mengine, Msemaji wa Ikulu ya Russia, Dmitry Peskov amelaani mazungumzo yaliyofanywa na maafisa wa Ujerumani kuhusu kuisusia Rissia akisema kuwa jambo hilo litazidi tu kutatanisha mambo.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin pia amesema kuwa, Russia inapokea kwa mikono miwili juhudi za kidiplomasia za kuweza kuutatua mgogoro wa Ukraine.