Walimwengu leo wanaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake
Dunia leo tarehe 8 Machi inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake ikiwa ni kampeni ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha juhudi za kuleta usawa wa kijinsia duniani kote.
Mwaka huu siku hii inaadhimishwa leo Ijumaa huku kaulimbiu ikiwa ni "Wekeza kwa wanawake: Ongeza kasi ya maendeleo."
Lengo la kuadhimisha siku hii kujaribu kuwezesha uthabiti wa kiuchumi wa wanawake, ambako kunaweza kuwa ni hatua chanya kufikia juhudi za usawa.
Jemimah Njuki, mkuu wa kitengo cha uwezeshaji wa kiuchumi katika shirika la wanawake la Umoja wa Mataifa, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni muhimu kwa sababu "dunia kwa kweli iko katika njia panda, kwa usawa wa kijinsia."
Aidha amebainisha kuwa duniani kote, haki za wanawake zinazidi kutishiwa, au kupiga hatua nyuma, hata katika maeneo ambayo viongozi walidhani wamepiga hatua chanya. Kulingana na na shirika la wanawake la UN Women, mwanamke mmoja kati ya 10 hii leo anaishi katika umaskini uliokithiri.
Ulimwengu unaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani leo huku Shirika la Kazi Duniani (ILO) likiripoti kuwa, wastani wa mshahara wa mwanamke kote duniani ni mdogo kwa asilimia 20 kulinganisha na wa mwanaume na kwamba, ufa uliopo baina ya mwanaume na mwanamke katika medani ya kazi haujapungua kwa kipindi cha miaka 20 sasa.
Dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa kutoa wito wa kushirikishwa zaidi tabaka hilo muhimu katika jamii katika taasisi za kuchukua maamuzi muhimu ya kitaifa na kimataifa, kulindwa haki zao na hadhi yao ya kibinadamu.