Umoja wa Mataifa: Mwaka 2023 ulikuwa mbaya kwa wahamiaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i109248-umoja_wa_mataifa_mwaka_2023_ulikuwa_mbaya_kwa_wahamiaji
Ripoti ya Shirika la Wahamiaji la Umoja wa Mataifa, (IOM) imeutaja mwaka 2023 kuwa mwaka mbaya zaidi kwa wahamiaji katika kipindi cha muongo mmoja.
(last modified 2024-03-07T22:51:49+00:00 )
Mar 07, 2024 22:51 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Mwaka 2023 ulikuwa mbaya kwa wahamiaji

Ripoti ya Shirika la Wahamiaji la Umoja wa Mataifa, (IOM) imeutaja mwaka 2023 kuwa mwaka mbaya zaidi kwa wahamiaji katika kipindi cha muongo mmoja.

Idadi ya vifo vya mwaka jana iliongezeka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka 2022.

Ripoti hiyo inasema, zaidi ya wahamiaji 8,500 walikufa mwaka jana duniani kote katika njia wanazotumia wahamiaji za ardhini na majini. Hiki ni kiwango cha juu zaidi tangu shirika hilo lilipoanza kuhesabu vifo vya wahamiaji muongo mmoja uliopita.

Shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva, Uswisi, limetahadharisha kuwa kuna uwezekano kwamba, hali halisi huenda ni mbaya zaidi, kwa kuzingatia kwamba si kila mhamiaji aliyepoteza maisha aliweza kupatikana taarifa zake katika ukusanyaji wa data.

Kwa ujumla, idadi kubwa zaidi ya vifo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa barani Asia, ambako zaidi ya wahamiaji 2,000 walikufa ikilinganishwa na wastani wa kila mwaka wa chini ya 1,000 tangu 2014.

Kupitia barua pepe, msemaji wa IOM, Jorge Galindo, amesema ongezeko la vifo barani Asia mwaka jana lilitokana na vifo miongoni mwa Waafghani wanaokimbilia maeneo jirani kama Iran pamoja na wakimbizi wa Rohingya kwenye njia za baharini.

 

Aidha shirika hilo limeongeza kwamba, idadi kubwa ya vifo vya wahamiaji, lilitokea kwenye njia hatari ya kuvuka Bahari ya Mediterenia na kuonesha umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kupoteza zaidi maisha ya watu.

Idadi hiyo pia inajumuisha wahamiaji waliotoweka ambao mara nyingi wanajaribu kuvuka bahari na kusadikiwa kuwa walikufa hata ikiwa miili yao haikupatikana.