Moscow: Marekani inaingilia uchaguzi wa wa Rais wa Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i109564-moscow_marekani_inaingilia_uchaguzi_wa_wa_rais_wa_russia
Uchaguzi wa Rais nchini Russia ulianza jana Ijumaa. Balozi wa nchi hiyo mjini Washington amelalamika kuwa Marekani inaingilia masuala ya ndani ya nchi yake yakiwemo yanayohusiana na uchaguzi huo.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Mar 16, 2024 07:46 UTC
  • Moscow: Marekani inaingilia uchaguzi wa wa Rais wa Russia

Uchaguzi wa Rais nchini Russia ulianza jana Ijumaa. Balozi wa nchi hiyo mjini Washington amelalamika kuwa Marekani inaingilia masuala ya ndani ya nchi yake yakiwemo yanayohusiana na uchaguzi huo.

Balozi Anatoly Ivanovich Antonov amenukuliwa na shirika la habari la FARS akisema kuwa Marekani inaendesha vitendo vya kigaidi dhidi ya Russia na inaingilia uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo.

Amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na vyombo vya habari vya Russia na kuongeza kuwa, Marekani inavizia fursa yoyote ya kuweza kuisababishia madhara Moscow ikiwa ni pamoja na kuchochea vitendo vya kigaidi dhidi ya nchi yake.

Balozi wa Russia mjini Washington ameongeza kuwa, viongozi wa Marekani wanajifanya kusahau kwamba Rais Vladimir Putin alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kujitolea kuisaidia Marekani baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11, 2001.

Russia inailalamikia Marekani kuwa inaingilia uchaguzi nchini humo

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia ameendelea kusema kuwa, Moscow haiwezi kukubaliana na mfumo wa kimataifa uliosimama kwenye sheria zilizowekwa na Marekani na inatambua vyema jinsi viongozi wa White House wanavyofanya uchochezi dhidi ya Russia.

Matamshi ya Balozi wa Russia nchini Marekani yametolewa katika hali ambayo, hivi karibuni viongozi wa ngazi za juu wa Marekani wameonekana kuingilia waziwazi uchaguzi wa Rais wa Russia ulioanza jana Ijumaa.

Hivi karibuni Balozi Antonov alizionya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kuwa zisiingilie masuala ya ndani ya Russia na zisijiingize kwenye vita ambavyo ni vigumu sana kutabiri hasara zake.

Vile vile amesema kuwa, vitendo vya viongozi wa Marekani havibashiri kupungua mivutano kati ya Washington na Moscow na ametabiri kuwa mivutano hiyo itaendelea kwa muda mrefu hadi White House itakapoacha uadui wake.