Mar 17, 2024 05:45 UTC
  • Trump aonya: Kutakuwa na 'umwagaji mkubwa wa damu' nisipochaguliwa kuwa rais wa Marekani

Donald Trump ameuambia mkutano wa hadhara katika jimbo la Ohio kwamba uchaguzi wa rais wa Novemba utakuwa "tarehe muhimu zaidi" katika historia ya Marekani akiitaja kampeni yake ya kuingia tena Ikulu ya White kama hatua ya mabadiliko muhimu sana kwa nchi hiyo.

Siku chache baada ya kunyakua nafasi ya kuwa mgombea urais mtarajiwa wa chama chake cha Republican, rais huyo wa zamani wa Marekani alionya pia juu ya alichokiita "umwagaji wa damu" ikiwa hatachaguliwa, ingawa haikufahamika alikuwa akimaanisha nini kwa kauli yake hiyo, sambamba na vitisho alivyotoa kwa sekta ya uundaji magari.
 
"Tarehe... kumbuka hii, Novemba 5... ninaamini itakuwa tarehe muhimu zaidi katika historia ya nchi yetu," alitangaza mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 akiwaambia hadhirina katika mkutano wa hadhara jana Jumamosi huko Vandalia, Ohio, sambamba na kurudia shutuma zake kwamba mpinzani wake, Rais Joe Biden, ndiye rais "mbaya zaidi", kuwahi kutokea katika historia ya Marekani.
 
Akikosoa kile alichosema mipango ya Wachina ya kuunda magari huko Mexico na kuwauzia Wamarekani, Trump alisema: "hawataweza kuuza magari hayo ikiwa nitachaguliwa".
 
Trump amesema: "sasa nisipochaguliwa itakuwa ni umwagaji mkubwa wa damu kwa watu wote, hilo litakuwa dogo zaidi, utakuwa umwagaji damu kwa nchi. Hilo litakuwa dogo zaidi. Lakini wao " hawatauza magari hayo."
Biden (kulia) na Trump

Mapema mwezi huu Trump na Biden kila mmoja alishinda wajumbe wa kutosha kushinda uteuzi katika vyama vyao katika kinyang'anyiro cha urais wa 2024, ili kuchuana tena kwa kuzindua moja ya kampeni ndefu zaidi za uchaguzi katika historia ya Marekani.

Miongoni mwa masuala ambayo Trump anayafanyia kampeni ni mageuzi makubwa ya kile anachokiita sera za uhamiaji za "onyesho la kutisha" la Biden, licha ya kufanikiwa kuwashinikiza Warepublican kuzuia mswada wa Bunge la Congress ambao ulijumuisha hatua kali zaidi za usalama za mpakani kuwahin kuchukuliwa katika miongo kadhaa.

Siku ya Jumamosi alichochea tena suala la mpaka alipowafikia wapiga kura wa jamii za wachache ambao kijadi hupigia kura chama cha Democrat.

Alisema Biden "amewachoma kisu mgongoni wapiga kura Wamarekani wenye asili ya Afrika kwa kutoa vibali vya kufanya kazi kwa "mamilioni" ya wahamiaji, akionya kwamba Wamarekani weusi na Wamarekani wenye asili ya Kilatini "ndio watakaoteseka zaidi."

Kwa miongo kadhaa Ohio imekuwa ikionekana kama jimbo la mpambano, ingawa imekuwa ikionekana zaidi kuwa ngome ya Republican tangu Trump alipoingia White House katika uachaguzi wa 2016.

Mkutano wa jana umefanyika siku moja baada ya makamu wa rais wa zamani wa Trump, Mike Pence, kusema hatamuidhinisha bosi wake wa zamani kwa muhula wa pili katika Ikulu ya White House.../

Tags