Jan 06, 2024 10:52 UTC
  • Kumbukumbu ya mwaka wa 3 tangu baada ya tukio la Januari 6; Ishara ya kufifia demokrasia ya Marekani

Maadhimisho ya miaka mitatu ya shambulio dhidi ya Bunge la Congress ya Marekani Januari 6, 2021 yamewadia huku wapinzani wawili katika uchaguzi wa rais, ambao ni Rais Mdemocrati, Joe Biden, na mgombea mkuu wa chama cha Republican, Donald Trump, wakishambuliana kwa maneno makali hasa katika kipindi hiki cha kuingia mwaka wa uchaguzi wa rais nchini Marekani.

Tukio hilo la Januari 6 limekuwa kiini cha mzozo kati ya wawili hao. Joe Biden ameonya kuhusu uwezekano wa kutoweka kabisa demokrasia ya Marekani iwapo Trump atachaguliwa tena kuwa rais wa nchi hiyo. Biden amemtuhumu Donald Trump na wafuasi wake kuwa wanazusha "machafuko ya kisiasa" na kusema kuwa, rais huyo wa zamani wa Marekani yuko tayari kuitoa kafara demokrasia ili arejee madarakani.
Trump amejibu mashambulizi ya maneno ya Joe Biden kwa kumwita Rais huyo wa Marekani kuwa ni "tapeli" na kumshutumu kwa kutokuwa na uwezo, kwamba ni mfisadi, dhaifu na aliyefeli. "Rekodi ya udhaifu wa Biden, uzembe, ufisadi na kufeli bado haijavunjwa", amesisitiza Donald Trump akizungumza katika jimbo la Iowa siku ya Ijumaa ya jana. 

Biden na Donald Trump

Shambulio dhidi ya jengo la Congress ya Marekani mnamo Januari 6, 2021 lilifanywa na kundi la wafuasi wa Donald Trump. Shambulio hilo lilivuruga kikao cha Congress kilichofanyika kwa ajili ya kuthibitisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020. Trump, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa rais wa Novemba 2020 na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden, alikuwa na nafasi muhimu katika tukio la Januari 6 kwa kuwachochea wafuasi na waungaji mkono wake kupinga matokeo ya uchaguzi huo kwa madai kwamba, kumefanyika wizi wa kura. Trump, akiwa rais mwenye jukumu la kulinda mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo, aliutaja mfumo huo kuwa mbovu na kimsingi alitilia shaka mfumo wa upigaji kura na uchaguzi wa Marekani.  Na kwa kusisitiza suala la kutokea udanganyifu mkubwa katika uchaguzi huo, kivitendo, Trump aliandaa mapinduzi kwa lengo la kuvuruga mchakato wa kisheria wa kutangazwa uraisi wa Joe Biden kwa kuwachochea wafuasi wake na kuwahimiza kufanya ghasia na kushambulia majengo ya Congress. Wakati wa shambulio hilo, watu 5 waliuawa, na Congress ikatumbukia katika machafuko makubwa. Hata hivyo, washambuliaji hao walishindwa kufikia lengo lao la kutwaa matokeo ya uchaguzi wa rais au kuchukua mateka mwanasiasa yeyote wa ngazi ya juu wa Marekani.

Idara ya upelelezi ya Marekani (FBI) na vyombo vingine vya kutekeleza sheria vililitaja tukio la Januari 6 kuwa ni kitendo cha ugaidi wa ndani ya nchi. Trump pia aliitwa na kusailiwa na Wademocrati kwa kauli zake za kichochezi alizozitoa kabla ya kushambuliwa jengo la Congress. Hata hivyo alinusurika jaribio la kumuuzulu baada ya Seneti kuingilia kati. Pamoja na hayo, Wizara ya Sheria ya Marekani imefuatilia kwa dhati na kuwafungulia mashtaka wahusika wa tukio hilo. Kufikia sasa, zaidi ya watu elfu moja wameshtakiwa katika kesi hii.

Congesi ya Marekani

Tukio la Congress tarehe 6 Januari lilikuwa kiashiria cha mwanzo wa enzi ya baada ya Marekani na kusahaulika mtindo na maadili ya Kimarekani, haswa katika uwanja wa demokrasia. Wakati huo huo, tukio hilo la Congress ni ishara ya jambo lisilopingika ndani ya Marekani, yaani, kuongezeka kwa pengo kati ya wahafidhina na Wanademokrati katika ngazi ya wasomi na mpasuko wa kambi mbili ndani ya jamii ya Marekani. Hadi hii leo bado kuna hitilafu za kimitazamo kati ya Wademokrati na Warepublican kuhusu sababu za tukio hilo na upande uliosababisha uhalifu huo.

Katika upande mwingine, shambulio dhidi ya Bunge la Congress mnamo Januari 6, 2020 limewafanya wachambuzi kuonya juu ya hatari halisi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Merekani, jambo ambalo halikuwa hata likifikirika miaka michache iliyopita. Barbara Walter, profesa wa sayansi ya siasa wa Marekani, amekiri waziwazi kwamba fikra ya kuwepo kwa mfumo wa kidemokrasia kwa maana yake halisi katika nchi yake ni dhana potofu, na ameonya kwamba Marekani inaelekea kwa kasi ya kustaajabisha kwenye ukosefu wa amani, vita vya ndani na mapinduzi. 

Tags