Jan 09, 2024 02:15 UTC
  • Ombi la Italia la kuunda jeshi la Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, amesema kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kuunda jeshi lake la pamoja ambalo linaweza kuwa na jukumu la kudumisha amani na kuzuia migogoro.

Tajani ameeleza kuwa ushirikiano wa karibu wa Ulaya katika nyanja za ulinzi ni kipaumbele kwa chama cha Forza Italia anachokiongoza na kusema: "Ikiwa tunataka kuwa walinzi wa amani duniani, tunahitaji kuwa na jeshi la Ulaya, na hili ndilo sharti la msingi la kuwa na sera kigeni yenye taathira ya Ulaya."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema: Katika ulimwengu ulio na wachezaji wenye nguvu kama Merekani, Uchina, India, Russia na machafuko kuanzia Mashariki ya Kati hadi kanda ya Indo-Pacific, raia wa Italia, Ufaransa au Slovenia wanaweza kulindwa tu na kile ambacho tayari kipo, yaani Umoja wa Ulaya." 

Ombi la Italia kama mwanachama muhimu wa Umoja wa Ulaya na NATO la kuundwa jeshi la Ulaya linaoana na maombi ya hapo awali kuhusiana na suala hili kabla ya vita kati ya Russia na Ukraine. Katika kipindi cha uongozi wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, watu wa Ulaya walifikia hitimisho kwamba kuna udharura wa kuundwa jeshi la pamoja la Ulaya na kuanzishwa chombo kinachojitegemea cha ulinzi barani humo kwa kizingatia mtazamo hasi Trump kuhusiana na NATO na ukosoa wake wa mara kwa mara kuhusu mchango mkubwa wa Washington katika shirika hilo la kijeshi na kuongezeka pengo na tofauti kati ya Ulaya na Marekani.

Donald Trump

Viongozi wa nchi muhimu za Ulaya yaani Ufaransa na Ujerumani walifikia hitimisho kwamba haiwezekani tena kuendelea kuitegemea Washington katika suala la kulinda usalama wa Ulaya kutokana na misimamo ya kimabavu na ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump, na kwamba Ulaya inapaswa kushughulikia usalama wake yenyewe.  Hasa, kwa kutilia maanani kwamba Trump alikuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba nchi wanachama wa NATO wa Ulaya zinapaswa kuongeza bajeti yao ya kijeshi, na wakati huo huo, alitaka kuongezwa mchango wao katika gharama za NATO. Wakati huo huo vitisho vya mara kwa mara vya Trump kuhusu kujiondoa Marekani katika NATO, ambavyo vililenga kuwajengea hofu watu wa Ulaya na kuwalazimisha kukubali masharti na matakwa ya Washington, viliimarisha azma ya wakuu wa Ujerumani na Ufaransa ya kuanzisha vyombo vinayojitegemea vya ulinzi na kijeshi haraka iwezekanavyo, haswa jeshi la Ulaya.  

Katika mkondo huo huo, mnamo Januari 2019, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alipendekeza wazo la kuundwa jeshi la Ulaya na kuanzisha muundo unaojitegemea wa usalama, ambalo lilikabiliwa na uipinzani mkali wa Trump. Wazo hilo liliungwa mkono waziwazi na Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, Angela Merkel.

Baada ya Joe Biden kuchukua madaraka Januari 2021 na juhudi zake za kurejesha uhusiano baina ya pande mbili za Bahari ya Atlantiki, msimamo mkali wa Washington kuhusu NATO ulipungua. Hata hivyo serikali ya Biden bado ilitaka kuongezwa bajeti ya kijeshi ya nchi za Ulaya. Kuzuka kwa vita vya Ukraine mnamo Februari 2022 na jitihada za wazi za Merekani za kuwa kiongozi wa kambi ya Magharibi na NATO dhidi ya Russia, pamoja na ongezeko kubwa la uwepo wa kijeshi wa Merekani huko Ulaya, vimeongeza utegemezi wa nchi za Ulaya kwa Washington katika nyanja za ulinzi na usalama, suala ambalo lilikuwa takwa la muda mrefu la Marekani.

Ukraine

Ingawa Merekani inaukubali Umoja wa Ulaya kama nguvu ya kiuchumi na inafanya miamala mikubwa ya kiuchumi, kibiashara na kifedha na EU, lakini daima imekuwa ikipinga kujitegemea kiulinzi Ulaya na kuundwa jeshi la ulinzi la Ulaya. Hapana shaka yoyote kwamba Biden pia atakuwa na mtazamo huo huo kuhusu suala la kuundwa jeshi la Ulaya.

Inatupasa kuashiria hapa kuwa jitihada za nchi za Ulaya katika nyanja za ushirikiano wa kiulinzi zimepanuka zaidi tangu baada ya kuuanza vita vya Ukraine, japo kuwa jitihada hizi zimejikita zaidi katika suala la kupanua shirika la kijeshi la NATO. Mwaka jana Finland ilijiunga na NATO, na Sweden inatarajiwa kujiunga na jumuiya hiyo mwaka huu wa 2024.

Kwa sasa Italia kama nchi muhimu mwanachana wa Ulaya na NATO unasisitiza sana suala la kuanzishwa jeshi la Ulaya, jambo ambalo ni mwendelezo wa juhudi za Ufaransa na Ujerumani katika uwanja huo.

Nukta muhimu ni kwamba Russia ambayo inakabiliana na vita mseto vya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, inapinga ombi la Italia la kuanzishwa jeshi la Uulaya. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema kuhusu suala hilo kwamba, kabla ya kuanzisha jeshi la pamoja, Ulaya inapaswa kwanza kufikiria jinsi la kutengeneza chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona au ijifunge jinsi ya kulinda mipaka yake kwa njia za kibinadamu.     

Tags