Mar 18, 2024 03:03 UTC
  • Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yaendelea kushuhudiwa katika nchi mbalimbali

Wananchi katika nchi mbalimbali kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano na mikusanyiko mbalimbali katika kuwaunga mkono na kuonyesha mshikamano kwa raia madhulumu wa Palestina.

Waungaji mkono wa Palestina wameandamana huko Paris mji mkuu wa Ufaransa wakitaka kusitishwa vita na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Ukanda wa Gaza. 

Waandamanaji hao wameituhumu serikali ya Ufaransa kwa kushiriki katika jinai za utawala wa Kizayuni unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza na kuitaka serikali ya Paris kuacha kutuma zana za kijeshi kwa utawala wa Kizayuni na kutoingiza Ufaransa bidhaa zinazozalishwa huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).  

Wakati huo huo wanafunzi wa sekondari na wa vyuo vikuu wanaoiunga mkono Palestina wameandamana katika mji wa Melbourne nchini Australia huku wakipiga nara za "Palestina ni lazima iwe huru" na "mapambano ya kuikomboa Palestina yanaendelea."  

Wauangaji mkono wa Palestina huko Toronto, Canada pia wamefanya maandamano mbele ya eneo palipofanyika harambee ya kukusanya misaada ya kifedha ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Justin Trudeau, na kumtuhumu kuwa anaunga mkono jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Palestina na kutoa wito wa kusitishwa mara moja vita huko Ukanda wa Gaza.

Tags