UNICEF: Israel inaendesha "vita vya kuwalenga watoto" wa Ghaza iliyowekewa mzingiro
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF James Elder amesema matukio yanayojiri katika Ukanda wa Ghaza ni "vita dhidi ya watoto," na kusisitiza kuwa eneo hilo hivi sasa si mahala pa kuishi watoto.

Amefafanua kwa kusema: "zaidi ya watoto 10,000 wameuawa, na idadi inaendelea kuongezeka. Hatujui ni wangapi wako chini ya vifusi. Hili ni balaa kubwa kwa watoto. Watoto wengi wana njaa, na baa la njaa limeshakaribia."
Msemaji wa UNICEF ameeleza pia kuwa watoto huko Ghaza wanakabiliwa na matatizo mengi ya kisaikolojia na kuongeza kwamba njia pekee ya kutibu watoto hao ni kuanza na "usitishaji mapigano."
Ametoa indhari kwa kusema: Ghaza si mahali salama kwa watoto hivi sasa wakati kuna watoto zaidi ya milioni moja katika eneo hilo. Kwa hivyo, inabidi upatikane usitishaji vita kwanza, na kisha kuhakikisha watoto hao wanapata huduma zote wanazohitaji.
Wapalestina wanaokaribia 32,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi na zaidi ya 74,000 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Ghaza tangu jeshi la utawala haramu wa Israel lilipoanzisha vita vya mashambulio ya kinyama na mauaji ya kimbari katika eneo hilo Oktoba 7, 2023.../