Mwanae bin Laden aitisha Marekani kuwa atalipiza kisasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i11011-mwanae_bin_laden_aitisha_marekani_kuwa_atalipiza_kisasi
Mwana wa kiume wa Osama bin Laden, kinara wa zamani wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ametuma ujumbe wa sauti na kuitishia Marekani kuwa, atalipiza kisasi damu ya baba yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2016 23:04 UTC
  • Mwanae bin Laden aitisha Marekani kuwa atalipiza kisasi

Mwana wa kiume wa Osama bin Laden, kinara wa zamani wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ametuma ujumbe wa sauti na kuitishia Marekani kuwa, atalipiza kisasi damu ya baba yake.

Kwa mujibu wa shirika la habari za kiintelijensia la SITE, Hamza bin Laden ametuma ujumbe wa sauti wa dakika 21 chini ya anwani ya "Sisi Sote ni Bin Laden" na kuusambaza katika intaneti. Katika ujumbe huo, Hamza bin Laden ameapa kuendeleza kile alichokitaja kuwa mapambano ya al Qaeda dhidi ya Marekani na waitifaki wake. Aidha amedai kuwa kundi la al Qaeda litaendelea kuilenga Marekani ndani na nje huku akiendelea kudai kuwa halipizi kisasi kwa niaba ya Osamba bin Ladin binafsi bali 'kwa niaba ya wale wote wanaotetea Uislamu'.

Osama bin Laden aliuawa mwaka 2011 akiwa mafichoni Pakistan katika shamulizi lililotekelezwa na makomando wa Marekani. Bin Laden alikuwa akisakwa na Marekani kutokana na kukiri kuwa alihusika na hujuma za kigaidi za Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Nyaraka zilizofichuka mwaka jana zilionyesha kuwa bin Laden alikusudia kumpa mwanawe Hamza, uongozi wa al Qaeda.

Bruce Riedel mtaalamu wa Shirika la Brookings anasema, Hamza, anayesadikiwa kuwa na umri wa miaka 25, ataipa al Qaeda utambulisho mpya unaofungamana na mwanzilishi wake.

Haya yanajiri wakati ambao mgombea kiti cha urais kwa tikiti ya Democrats nchini Marekani Hillary Clinton amekiri wazi kuwa Marekani ndiyo iliyoanzisha kundi la Kiwahhabi la Al Qaeda kwa ajili ya kufikia malengo yake huko Afghanistan. Aidha tume iliyochunguza matukio ya Septemba 11 Marekani imesema watawala wa Saudia ambao ni waitifaki wa Marekani walikuwa na nafasi kubwa katika hujuma za kigaidi dhidi ya majengo mawili pacha huko York na jengo la Pentagon mjini Washington. Hayo yamo katika "kurasa 28" kuhusu tukio la Septemba 11 ambazo mkuu wa CIA amesema itakuwa bora iwapo hazitowekwa hadharani.

Saudi Arabia ilitishia kwamba endapo nyaraka hizo zitawekwa hadharani itaondoa mitaji yake ya mabilioni ya dola katika benki za Marekani.