Mar 31, 2024 11:28 UTC

Wananchi huko Italia, Norway, Marekani, Japan na Morocco kwa mara nyingine tena wameandamana kulaani mauaji ya kimbari ya raia wa Palestina yanayofanywa na wanajeshi ghasibu wa utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la Iran Press limeripoti kuwa maelfu ya wananchi wa Italia wamemiminika katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa nchi hiyo Rome huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yenye maandishi ya kuwaunga mkono wakazi wa Ukanda wa Gaza na mapambano ya ukombozi wa Palestina. Wafanya maandamano hao wametaka kusitishwa vita na kufikiwa mapatano ya usitishaji vita haraka iwezekanavyo huko Ukanda wa Gaza.  

Wakati huo huo Wahadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali vya Italia zaidi ya 1,500 pia wametaka kusimamishwa ushirikiano wa kielimu na kivyuo vikuuu kati ya nchi hiyo na utawala bandia wa Kizayuni. 

Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Italia kikiwemo Chuo Kikuu kikubwa cha Rome pia wameandamana kuupinga utawala ghasibu wa Kizayuni na kukitaka chuo kikuu hicho kuacha kushirikiana katika masuala ya kielimu na utawala wa Israel. 

Jana Jumamosi pia wananchi katika mabara matatu ya dunia walifanya maandamano ya kuwaunga mkono raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza na kulaani jinai na mauaji ya kimbari ya  utawala wa Kizayuni katika eneo hilo. 

Huko kaskazini mwa Afrika yaani nchini Morocco wananchi wamefanya maandamano makubwa kulaani vita vya utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 

Maandamano ya Wamorocco kupinga mauaji ya kimbari ya Israe Ukanda wa Gaza 

Na huko Oslo mji mkuu wa Norway pia wakazi wa mji huo wameandamana ili kuonyesha mshikamano wao na wananchi wa Palestina. Wametaka kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza.   

Tags