Apr 20, 2024 02:59 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Mahesabu mabaya Asia Magharibi yatasababisha janga kwa dunia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu hali ya sasa katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, kosa moja la kimahesabu yumkini likasababisha maafa kwa eneo hilo na dunia nzima kwa ujumla.

Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kile kinachoendelea eneo la Magharibi mwa Asia kutokana na jinai za Wazayuni huko Gaza na kusema eneo hilo liko kwenye ukingo wa shimo.

Guterres ameongeza kuwa, kushadidi mizozo katika eneo hilo kunazidisha umuhimu wa kuunga mkono juhudi za nia njema za kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Asia Magharibi na kuundwa taifa huru la Palestina kuliko wakati mwingine wowote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasisitizia Wazayuni kwamba kusitisha ukatili na vita katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kukomesha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kutapunguza kwa kiasi kikubwa mivutano katika eneo hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo baada ya Marekani, ambayo ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, imeendeleza sera yake ya kudhoofisha kupatikana haki za Wapalestina kwa kutumia vibaya haki yake ya kura ya turufu na kukwamisha azimio la kuipatia Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Katika upigaji kura huo, nchi 12 wanachama wa Baraza la Usalama la UN zilipiga kura za kuunga mkono, Uswisi na Uingereza zilipiga kura ya kutopinga au kuunga mkono upande wowote; na Marekani ikazuia kupitishwa azimio hilo kwa kulipigia kura ya turufu.

Tags