Apr 22, 2024 06:18 UTC
  • Hamu ya Wamarekani kupiga kura imepungua kwa kiwango kisicho na mfano

Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Chaneli ya NBC News umeonyesha kuwa, Wamarekani wanapoteza hamu ya kupiga kura katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu kwa sababu mgombea wa chama cha Democrat Joe Biden na mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump, wote wawili hawana mvuto kwa wapiga kura.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kuwa, ni 38% tu ya wapiga kura wa Marekani wana mtazamo chanya kuhusu Biden. Aidha, asilimia sawa na hiyo ya wapiga kura, kwa tofauti ndogo tu wana mtazamo chanya kuhusu Trump.

Jeff Horwitt, msimamizi wa uchunguzi wa maoni wa chama cha Democratic aliyesaidia kufanikisha zoezi hilo lililoendeshwa na NBC News amesema: "Wamarekani hawakubaliani sana siku hizi, lakini hakuna kitu kinachounganisha nchi zaidi sasa hivi kama hamu ya wapiga kura kuupuuza uchaguzi huu".

Naye Bill McInturff, msimamizi wa uchunguzi huo wa maoni wa NBC kutoka chama cha Republican, amesema, matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa idadi ya wapiga kura itakuwa ndogo mnamo mwezi Novemba, hasa miongoni mwa vijana.

Amefafanua kuwa, ni asilimia 36 pekee ya wapiga kura walio na umri wa chini ya miaka 35 walio na hamu kubwa ya kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Wakati 70% ya Warepublican na 65% ya Wademocrat wanavutiwa sana na mchuano wa marudiano baina ya Biden na Trump, ni 48% tu ya wapigakura wasio na vyama wanavutiwa na suala hilo.

Uchunguzi huo wa maoni umeonyesha pia kuwa Trump amemtangulia Biden kwa tofauti ndogo ya 46% kwa 44% endapo watachuana peke yao. Lakini kama wagombea wa ziada watajumuishwa, Biden atampita Trump kwa asilimia 39 kwa 37 ya kura. Na sababu ni kuwa Trump atapoteza wapiga kura wengi zaidi ambao wangempigia yeye kama kutakuwa na chaguo jengine ghairi ya Biden.../