Majaji Wakuu wa Jumuiya ya Shanghai wamuenzi Shahidi Raisi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i112088-majaji_wakuu_wa_jumuiya_ya_shanghai_wamuenzi_shahidi_raisi
Majaji Wakuu na Wenyeviti wa Mahakama za Juu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) wamenyamaza kimya kwa dakika moja kumuenzi Shahidi Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maafisa wenzake walioaga dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran.
(last modified 2024-05-23T06:55:05+00:00 )
May 23, 2024 06:55 UTC
  • Majaji Wakuu wa Jumuiya ya Shanghai wamuenzi Shahidi Raisi

Majaji Wakuu na Wenyeviti wa Mahakama za Juu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) wamenyamaza kimya kwa dakika moja kumuenzi Shahidi Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maafisa wenzake walioaga dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran.

Viongozi hao wa mihimili ya Mahakama ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, wakati wa kuanza kikao cha ngazi ya juu leo Alkhamisi huko mjini Tashkent nchini Uzbekistan, wamemuenzi na kutoa heshima zao za mwisho kwa Sayyid Raisi na maafisa wengine waliokufa shahidi katika ajali hiyo ya Jumapili.

Shirika la habari la IRNA limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, Kazem Gharibabadi, Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Kibinadamu la Iran ameongoza ujumbe wa maafisa wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye mkutano huo mjini Tashkent.  

Weledi wa mambo wanasisitiza kuwa, uwepo amilifu wa Iran kwenye Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) na hata Kundi la BRICS ni ithibati na ishara ya kufeli na kusambaratika sera ya kuitenga Iran kimataifa.

Kufuatia kufa shahidi Rais wa Iran Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi, nchi nyingi duniani zimetangaza maombolezo ya kitaifa, huku viongozi wa kimataifa wakiendelea kutoa salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Iran.