May 26, 2024 10:05 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakaribisha uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Dharura na Kibinadamu amekaribisha hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ inayoutawala utawala wa Kizayuni usimamishe mara moja operesheni za kijeshi katika mji wa Rafah Kusini mwa Gaza.

Martin Griffiths, amekaribisha azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) la kuwalinda wafanyakazi wa mashirika yanayohusika katika masuala ya kibinadamu, pamoja na uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kutaka kusimamishwa operesheni ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji wa Rafah na kufunguliwa tena kivuko cha Rafah na akasisitiza kwamba, sheria za vita ambazo kila mtu anatakiwa kuzifuata, ni lazima ziheshimiwe.

Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Dharura na Kibinadamu.

Griffiths ameeleza kuwa, operesheni ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni huko Rafah ni janga lisiloelezeka na kuongeza kuwa, operesheni za ardhini za utawala huo zimewakosesha makazi Wapalestina zaidi ya laki nane waathirika wa vita waliokuwa wamekwenda kutafuta hifadhi katika mji huo wa Rafah kusini mwa Gaza kwa kuwafanya wakimbilie kwenye maeneo yasiyo na pa kukaa, maji, wala suhula na huduma za Afya.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, ingawa utawala haramu wa Israel umetupilia mbali miito ya jamii ya kimataifa ya kutoshambulia Rafah lakini maandamano yaliyofanywa kila pembe ya dunia ya kutaka kusitishwa mara moja shambulio hilo hayawezi kupuuzwa.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kufunguliwa tena vivuko vyote vya ardhini ili kuusaidia ipasavyo Ukanda wa Gaza.


Mahakama ya Kimataifa ya Haki yenye makao yake makuu mjini The Hague, ambayo ni chombo cha juu zaidi cha kimahakama cha Umoja wa Mataifa, siku ya Ijumaa tarehe 24 Mei ilitoa hukumu ya kuutaka utawala haramu wa Israel usitishe mara moja mashambulizi ya kijeshi dhidi ya mji wa Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza.

Kwa kura 13 za 'ndiyo' dhidi ya kura 2 za 'hapana', mahakama hiyo iliamuru kusitishwa mara moja operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni huko Rafah na kutaka kufunguliwa tena kivuko cha Rafah kwa ajili ya kuingiza misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Nchi na asasi mbalimbali za kimataifa na za kieneo zimekaribisha hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki inayoamuru kusimamishwa mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Rafah, kufunguliwa tena kivuko hicho kwa ajili ya kuingizwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, kutolewa hakikisho la kuingia kamati ya kutafuta ukweli ili kubaini uhakika wa mauaji ya kimbari huko Gaza na kuwasilisha ripoti husika katika muda wa mwezi mmoja kutoka sasa.
Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) amesisitiza kuwa hukumu ya Mahakama ya The Hague kuhusu Israel kusitisha operesheni za kijeshi huko Rafah ina ulazima wa kutekelezwa na pande zote zinapaswa kuifuata.