May 27, 2024 05:56 UTC
  • Watu 670 wapoteza maisha katika maporomoko ya udongo Papua New Guinea

Maporomoko ya udongo huko kaskazini mwa Papua New Guinea yamepelekea watu wasiopungua  670 kupoteza maisha na kijiji kizima kuangamizwa.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa jamii katika Kijiji cha Yambali, kilichoko chini ya mlima huko jimbo la ndani zaidi la Enga, iilifukiwa chini ya udongo Ijumaa kwenye kina cha kati ya mita sita hadi nane.

Serhan Aktoprak, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM amesema wafanyakazi sita wa shirika hilo wa kutoa huduma za misaada sambamba na watumishi wengine kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na serikali wako katika eneo hilo kutoa huduma za dharura.

IOM imesema miamba inayoendelea kuporomoka inakwamisha huduma za usaidizi na uokozi.

Maporomoko hayo ya udongo yamefurusha takribani watu 1,000 kutoka kwenye makazi yao na kuna hofu kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

Wakati huo huo, kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma salamu zake za mshikamano na watu wa Papua New Guinea kufuatia maporomoko hayo makubwa ya udongo ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu huku akisema watumishi wa Umoja wa Mataifa wako sambamba na serikali kusaidia juhudi za uokozi. Papua New Guinea ni nchi ya kisiwa iliyoko kwenye Bahari ya Pasifiki.