Ulimwengu wa Spoti, Juni 10
Hujambo mpenzi msikilizaji, natumai u mzima wa afya. Karibu tuangazie baadhi ya matukio makuu yaliyoshuhudiwa viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.
Soka: Iran yaizaba Hong Kong
Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeinyuka Hong Kong kwenye mchuano wa mkondo wa pili wa mechi za kuwania kufuzu finali zijazo za Kombe la Dunia. Katika mechi hiyo iliyipigwa Alkhamisi katika Uwanja wa Taifa Wa Hong Kong, Iran ikiipigia ugenini iliizaba mwenyeji mabao 4-2 katika mchezo huo wa Kundi E wa mzunguko wa kwanza wa kusaka tiketi za kushiriki Kombe la Dunia 2026.
Kwa ushindi huo, vijana wa Iran wamefikisha alama 13 na kujikita barabara kileleni mwa Kundi E, huku Hong Kong ikivuta mkia kundini kwa alama 1.
Iran bingwa wa badminton Asia ya Kati
Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Vijana ya Badminton 2024 ya eneo la Asia ya Kati yaliyofanyika mjini Shymkent, Kazakhstan. Mabarobaro hao wa Kiirani wametwaa medali 7 za dhahabu, 3 za fedha na moja ya shaba kwenye mashindano hayo ya kieneo. Baadhi ya vijana wa kike na kiume wa Iran waliotwaa medali za dhahabu katika kategoria mbali mbali kwa vijana wenye umri wa miaka 15 na 17 ni pamoja na Amirhossein Behjati Ardakani, Amirali Hatami, Amirali Ahmadloo, Bahar Gharibi na Mobina Salari Kor.
Kwengineko, timu ya taifa ya wanawake ya Kurash imekuwa mshindi wa pili katika Mashindano ya Kurash ya Asia. Timu hiyo imeshinda medali 2 za dhahabu, 3 za fedha na 3 za shaba katika kitengo cha timu na kuwa mshindi wa pili katika Michezo ya Asia ya Tehran, Iran. Kurash ni aina ya mieleka ya kale iliyoanzishwa zaidi ya miaka elfu 3,500 iliyopita katika eneo la Asia ya Kati hasa Uzbekistan na Tajikistan ya sasa.
Starlets ya Kenya shibri moja kutinga Kombe la Dunia
Timu ya soka ya Kenya ya wanawake walio chini ya umri wa miaka 17 'Junior Starlets' inajongea kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu, baada ya kuvuna ushindi wa aina yake wa mabao 3-0 dhidi ya Burundi. Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza wa raundi ya nne ya kuwania tiketi ya kufuzu, ilichezewa katika uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, Ethiopia mnamo Jumapili, ambapo mabanati hao wa Kenya walivuna ushindi mnono. Mshambuliaji Lorna Faith alikuwa wa kwanza kucheka na nyavu katika dakika ya 11 ya mchezo, kabla ya kiungo wa kati Marion Serenge kuongeza bao la pili kunako dakika ya 43, huku mtoka benchi Susan Akoth akifunga bao la tatu dakika ya 71 na kupatia Kenya pointi zote muhimu ugenini. Mkufunzi wa timu hiyo amewaasa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwashabikia akina dada hao watakapoupigia nyumbani katika mechi ya marudiano katika Uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, Jumapili ijayo ya Juni 16. Katika mechi nyingine barani Afrika, Zambia iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Morocco Jumamosi kwenye Uwanja wa Heroes huko Lusaka, Zambia. Mshambuliaji wa Zambia Namute Chileshe alifunga mabao katika dakika ya 13, 24 na 82. Goli la Morocco lilifungwa na Azraf Kautar kunako dakika ya 37. Timu tatu-bora kutoka kwenye mechi za kufuzu za eneo la Afrika, zitawakilisha bara hili kwenye Kombe la Dunia ambapo timu 16 kutoka mashirikisho sita zitawania taji. Mashindano ya Kombe la Dunia yatafanyika katika Jamhuri ya Dominika kuanzia Oktoba 16 hadi Novemba 3, 2024.
Dondoo za Hapa na Pale
Inaarifiwa kuwa, uongozi wa klabu ya Singida Black Stars (Ihefu) ya Tanzania umeanza mazungumzo ya kumpata beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe kwa lengo la kuwaongezea nguvu kwa msimu ujao wa mashindano. Kapombe aliyeichezea Simba kwa misimu saba mfululizo tangu aliposajiliwa 2017-2018 akitokea Azam FC, sambamba na nahodha John Bocco, Erasto Nyoni na kipa Aishi Manula, ni mmoja ya wachezaji wanaodaiwa wanaweza kutemwa Msimbazi, licha ya kuwa na mkataba hadi Juni mwakani kutokana na fagia fagia iliyoanza kupitishwa Msimbazi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ wamesema hawajajiuzulu na hawana mpango wa kujiuzulu nafasi zao, huku mvutano wa uongozi ukitokota kwenye uongozi wa klabu hiyo. Inadokezwa kuwa, mwekezaji na Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji, anatarajiwa kuwa sehemu ya wafanya uamuzi ndani ya klabu hiyo ikiwa pamoja na kusimamia usajili wa wachezaji kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Naye mwanachama wa Simba, Hamis Kigwangala ameweka wazi kuwa Mohamed Dewji haidai chochote klabu hiyo ya kandanda kwa mujibu wa mkataba. Aidha Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X akichangia mjadala uliotamalaki hivi sasa mtandaoni kuhusu migogoro ya klabu ya Simba, ameomba kupewa klabu hiyo kwa miezi 12 tu. Kadhalika, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC amesema kwa sasa akili yao wameielekeza kusaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao na si kingine. Amesema mambo yote ya klabu, ikiwemo usajili yatajulikana baada ya msimu kumalizika.
Na inaarifiwa kuwa, Thomas Tuchel alikutana na Sir Jim Ratcliffe karibuni kujadili uwezekano wa kuchukua nafasi ya Erik ten Hag kama meneja wa Manchester United.
………………….MWISHO…………….