Jun 17, 2024 08:07 UTC
  • Ombi la Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa la utawala wa Israel kuwekewa vikwazo vya kisiasa na kiuchumi

Akiashiria kwamba njaa ya hivi sasa huko Gaza ni moja ya njaa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mwanadamu amesema Israeli ilianzisha kampeni kubwa mnamo Oktoba mwaka uliopita kwa ajili ya kuwaweka njaa watu wa Palestina ambapo wengi wao hasa watoto wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na baa hilo la njaa ya kulazimishwa. Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula amesema wataalamu huru wa kimataifa wanayachukulia matukio ya sasa huko Gaza kuwa ni mauaji ya halaiki, n

Sisitizo la Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula, juu ya ulazima wa utawala wa kibaguzi wa Israel kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa linatolewa katika hali ambayo mashinikizo ya kisiasa na maombi ya mara kwa mara kwa utawala huo usitishe vita, mauaji ya kimbari na matumizi ya silaha ya njaa dhidi ya Wapalestina wasio na hatia kwa ajili ya kukiangamiza kizazi hicho, yameshindwa kuzaa matunda yanayotakikana.

Licha ya kupitishwa azimio dhidi ya utawala huo katika Baraza la Usalama siku Jumatatu, Juni 10, ambalo lilionyesha wazi takwa la jumuiya ya kimataifa kwa Tel Aviv la kutoendeleza mauaji ya umati  huko Gaza, lakini utawala huo umepuuza azimio hilo na sheria nyingine nyingi za kimataifa, na kuendeleza jinai na mauaji hayo dhidi ya Wapalestina wasio na hatia kwa uungaji mkono wa Marekani. Huku akionyesha ujeuri na kiburi cha kupindukia katika matamshi yake, Reut Shapir Ben-Naftaly, mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, amesema Tel Aviv itaendelea na operesheni zake za kijeshi na mauaji ya umati huko Gaza na wala haitajihusisha na mazungumzo aliyoyataja kuwa "yasiyo na maana" na Hamas.

Kwa kuzingatia hayo, licha ya kuwa jumuiya ya kimataifa imekaribisha kupitishwa azimio nambari 2735 la Baraza la Usalama, ambalo linataka kusitisha mapigano huko Gaza, azimio ambalo Hamas pia imelikubali, lakini Tel Aviv imelipinga na kusisitiza kuendelea kuua kwa umati raia wa Palestina. Kwa kuzingatia msimamo huo wa Israel, mwakilishi wa Russia amesisitiza kwamba azimio hilo limepuuzwa na utawala huo, sawa kabisa na unavyofanya kuhusiana na maazimio megine mengi ya Baraza la Usalama.

Ingawa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yana nguvu ya utekelezaji kisheria, lakini Israel imepuuza maazimio yoyote ya baraza hilo yanayohusiana na vita vya Gaza, yaani maazimio nambari 2712, 2720, 2728 na 2735, kwa kisinsingizio cha kutokuwepo taratibu zinazohitajika kwa ajili ya kuyatekeleza.

Kwa mujibu wa vipengee vya VI na VII vya Hati ya Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama lina mamlaka ya kupitisha maazimio mbalimbali. Kuhusu maazimio nambari 2712, 2720 na 2728 ya Baraza la Usalama, tunaelewa kwamba maazimio haya, hayana dhamana yoyote ya utekelezwaji ima kupitia nyenzo za kijeshi au zisizo za kijeshi kama vile vikwazo vya kiuchumi na mzingiro, kutokana na ukweli kwamba yamepitishwa kwa msingi wa kipengee cha VI ambacho hakijaainisha mchakato wa kutekelezwa kivitendo maazimio hayo. Kipengee hicho kinasisitiza tu kusuluhishwa mizozo kati ya pande mbili kupitia mazungumzo, upatanishi, mashirika ya kikanda au njia nyingine yoyote ya amani ili kusaidia kutatua hitilafu zilizopo.

Kwa maelezo hayo, ni wazi kwamba azimio jipya la Baraza la Usalama, yaani, azimio nambari 2735, limejumuishwa katika maazimio mengine ya huko nyuma yanayohusiana na Palestina, ambayo hayana dhamana yoyote ya utekelezwaji kivitendo.

Hivi sasa, kutokana na kuzorota hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, inaonekana kuwa hakuna chaguo jingine lililobakia isipokuwa kuuwekea utawala wa kigaidi wa Israel kila aina ya mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa ili kuulazimisha usitishe vita na mauaji ya umati dhidi ya watu wasio na ulinzi huko Gaza. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika taarifa yake Jumamosi, lilionya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika ukanda huo na kutangaza kuwa pamoja na kuendelea kuzuiwa kuingia misaada ya kibinadamu Gaza, zaidi ya watoto 50,000 wa ukanda huo wanakabiliwa na utapiamlo mkali. Taarifa ya shirika hilo, inaeleza kuwa mbali na suala hilo wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na njaa kali. Aidha kwa kutilia maanani vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni, hasa mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina, idadi ya mashahidi na waliojeruhiwa huko Gaza, ambapo wengi wao ni watoto na wanawake, imeongezeka sana na kupindukia watu elfu 120.