Jun 19, 2024 12:17 UTC
  • Russia: Ukraine katu haitajiunga na shirika la kijeshi la NATO

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema ni jambo lisiloyumkinika kwa Ukraine kuwa mwanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO.

Sergey Ryabkov amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la TASS na kuongeza kuwa, sharti lililotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa NATO kwa Ukraine ili nchi hiyo iruhusiwe kujiunga na jumuiya hiyo ya kijeshi linaonesha kuwa, haiwezakani kwa Kiev kujiunga na muungano huo.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg alisema hivi karibuni kuwa, ili Ukraine ikubaliwe kujiunga na muungano huo wa kijeshi wa Magharibi, sharti ishinde vita dhidi ya Shirikisho la Russia.

Ryabkov ameashiria msimamo huo wa Stoltenberg na kusema kua: Sharti hilo linamaanisha kuwa kamwe Ukraine haitawahi kujiunga na NATO, natumai Bwana Stoltenberg analifahamu hili.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg

Kabla ya hapo pia, Stoltenberg alisema muungano huo wa kijeshi wa Wamagharibi hauna mpango wa kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine, na kwamba jumuiya hiyo ya kijeshi haiitazami Russia kama tishio la kijeshi kwa nchi za Magharibi. 

Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya nchi za Magharibi  zinataka kutumwa askari wa NATO nchini Ukraine, lakini zingine zinasisitiza kuwa haziungi mkono mpango huo zikionya kuwa, hatua hiyo inaweza kuzusha Vita vya Tatu vya Dunia.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekuwa akiwashinikiza viongozi wa Magharibi waipe Kiev silaha na vifaa zaidi vya kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Moscow.

Tags