Erdogan: Nchi za Magharibi zimekuwa mateka wa mtu kichaa kama Netanyahu
(last modified Thu, 27 Jun 2024 02:58:39 GMT )
Jun 27, 2024 02:58 UTC
  • Erdogan: Nchi za Magharibi zimekuwa mateka wa mtu kichaa kama Netanyahu

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alisema jana Jumatano kwamba nchi yake inasimama bega kwa bega na Lebanon kutokana na mvutano unaozidi kuongezeka na utawala wa Kizayuni wa Israel, na amezitaka pande za kikanda kumuunga mkono katika msimamo huo.

Erdogan amezishutumu nchi za Magharibi kuwa zinaunga mkono mipango ya Israel ya "kupanua wigo wa vita katika eneo la Magharibi mwa Asia.”

Rais wa Uturuki amesema, akihutubia mkutano wa bunge wa chama tawala cha Haki na Maendeleo katika mji mkuu, Ankara, kwamba Israel kwa sasa inaangazia Lebanon, na madola ya Magharibi yanaonekana kuiunga mkono na kuiimarisha nyuma ya pazia.

Rais wa Uturuki ameonya kwamba mipango ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ya kupanua wigo wa vita inaweza kusababisha "maafa makubwa," akiongeza kuwa uungaji mkono wa Magharibi kwa Israel "unasikitisha."

"Inasikitisha sana kuona kwamba nchi zinazozungumzia uhuru, haki za binadamu na uadilifu zimekuwa mateka wa mtu kichaa kama Netanyahu," amesisitiza Erdogan.

Ameendelea kusema kwamba, picha za watoto wanaosumbuliwa na njaa katika Ukanda wa Gaza ni "fedheha kwa ulimwengu wa kisasa," na amezishambulia nchi za Kiislamu, akisema: "Hii pia itakumbukwa kama ishara ya udhaifu wa Ulimwengu wa Kiislamu."

Watoto wa Gaza

Rais wa Uturuki ametoa wito kwa Ulimwengu wa Kiislamu na nchi za Mashariki ya Kati kukabiliana na mipango hiyo ya umwagaji damu ya Israel.