Uhispania: NATO inapaswa kuacha undumakuwili kuhusu Ukraine na Gaza
Waziri Mkuu wa Uhispania ametoa wito kwa wanachama wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuheshimu sheria za kimataifa kwa kiwango sawa kuhusiana na Gaza na Ukraine bila "kutumia misimamo na sera za kindumakuwili".
Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Uhispania, amesema kuwa katika taarifa ya mwisho ya Mkutano wa NATO huko Washington, Ukraine imetajwa zaidi ya mara 60 na Gaza haikutajwa hata mara moja, na amewataka viongozi wa shirika hilo la kijeshi kuheshimu sheria za kimataifa kuhusiana na Gaza kama wanavyotaka wao sheria hizo ziheshimiwe nchini Ukraine.
Sanchez amesisitiza kwamba, ni muhimu sana kwa raia wa Uhispania kuelewa kwamba serikali ya nchi yao sio tu kwamba imetetea sheria za kimataifa kuhusu Gaza na Ukraine, lakini pia ina msimamo thabiti wa kisiasa na inaepuka sera za kinafiki na kindumakuwili.
Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kuwa Ukanda wa Gaza umeharibiwa kabisa na ujenzi wake mpya utachukua miongo kadhaa. Ameongeza kuwa, watu wengi wa Gaza wamelazimika kukukimbia makazi yao, na migogoro na maafa ikiwa ni pamoja na njaa kali, imeligubika eneo hilo.
Mwezi Mei mwaka huu Uhispania, Ireland na Norway zilipasisha rasmi mpango wa kutambua rasmi Palestina, hatua ambayo imeongeza himaya na uungaji mkono kwa Palestina barani Ulaya.
Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa NATO ulimaliza kazi zake jana mjini Washington huko Marekani kwa kutangaza kifurushi kipya cha misaada ya kiijeshi kwa Ukraine katika vita vyake dhidi ya Russia.