Msimamo wa wawakilishi wa nchi tofauti katika Baraza la Usalama la UN dhidi ya utawala wa Kizayuni
Wawakilishi wa nchi tofauti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Matafa wametoa radiamali yao kwa jinai za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza.
Riyad Mansour Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kuwa: 'Kile kinachojiri katika Ukanda wa Gaza kwa upande wa mauaji kimesajiliwa kama mauaji ya kimbari yaliyorekodiwa zaidi duniani.'

Ali Bagheri Kani Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema katika kikao hicho kuwa: Tunaliomba Baraza la Usalama litekeleze majukumu yake kama yalivyobainishwa katika Hati ya Umoja wa Mataifa kwa kuchukua hatua za dharura na za kivitendo ikiwemo kupasisha azimio kuu na lazima kutekelezwa ili kuulazimisha utawala wa Israel usitishe haraka iwezekanavyo mauaji ya kimbari na jinai zake za kivita dhidi ya Gaza.
Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia amesema katika kikao hicho cha Baraza la Usalama kuhusu Palestina kwamba: 'Marekani imekuwa mshirika wa moja kwa moja wa Israel katika vita dhidi ya Gaza kwa kuupatia utawala huo silaha za kuishambulia Gaza.' Lavrov pia ameutuhumu utawala wa Kizayuni kwa kutekeleza adhabu ya pamoja kwa kuendeleza vita na kuwazingira watu wa Gaza.
Pamoja na kuwa nchi mbalimbali katika Baraza la Usalama zimedhihirisha msimamo huru dhidi ya utawala wa Kizayuni na kusisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa jinai za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza, lakini viongozi wa Marekani wanaendelea kuihami na kuiunga mkono kwa pande zote Tel Aviv huku wakijaribu kuficha na kukanusha jinai za utawala huo haramu dhidi ya Gaza.
Linda Thomas-Greenfield Mwakilishi na Balozi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ambaye nchi yake inaunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina amejifanya kusikitishwa na kusema kwa unafiki kwamba: 'Raia wa Gaza wanaishi kuzimu.' Greenfield pia amezungumzia kupasishwa mipango ya utawala wa Kizayuni kwa lengo la kujenga maelfu ya makazi kwa ajili ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuongeza kuwa: 'Hatua hizi za upande mmoja haziwiani na sheria za kimataifa, na ni kwa madhara ya kupatikana suluhisho la serikali mbili.'

Viongozi wa Marekani wanatoa madai haya ya kujifanya wanasikitishwa huku eti wakiukosoa utawala wa Kizayuni katika hali ambayo Washington kivyovyote vile haiko tayari kusitisha na kuacha kuiunga mkono Tel Aviv; na ni mshirika wa Wazayuni katika jinai za mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kwa hatua yake ya kuufadhili kifedha na kuuhami pakubwa kwa silaha utawala huo ghasibu.
Utawala wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi yasiyo ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kufuatia uungaji mkono na himaya endelevu ya White House na kimya cha viongozi wa Marekani mkabala wa mashambulizi na jinai za kinyama za utawala huo ambazo hadi sasa zimepelekea kuuliwa shahidi makumi ya maelfu ya Wapalestina na kuharibu kikamilifu miundombinu ya eneo hilo. Tume huru ya haki za binadamu ya Palestina imetangaza katika taarifa yake kuwa raia wa Gaza wanakabiliwa na mateso na masaibu makubwa baada ya oparesheni ya kijeshi ya maghasibu wa Kizayuni katika mji wa Rafah na kukidhibiti kivuko cha Rafah.

Nchi huru duniani hazijakaa kimya mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni kinyume na serikali za Magharibi, ambapo zimeunga mkono kesi dhidi ya viongozi wa utawala huo katika Mahakama za Kimataifa kwa tuhuma za mauaji ya kimbari. Gaza imekuwa sehemu ya kuzingatiwa na jamii ya kimataifa kutokana na kuendelea mchakato wa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo; na kufuatiliwa jinai za viongozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni leo hii limekuwa takwa la kimataifa.
Uungaji mkono wa viongozi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni pia utazidisha tu hasira na ghadhabu za fikra za waliowengi ulimwenguni kwa Marekani na muitifaki wao wa siku zote yaani Tel Aviv. Wanaharakati wa kiraia na baadhi ya waungaji mkono wa Palestina huko Marekani pia wametahadharisha kuhusu taathira za sera za Washington na kusisitiza kuwa kuunga mkono utawala wa Israel ni aina fulani ya kushiriki katika jinai za Wazayuni.