Jul 23, 2024 02:23 UTC
  • Biden ajitoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais wa Marekani

Hatimaye, Joe Biden, Rais wa Kidemokrati wa Marekani mwenye umri wa miaka 81, amejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais wa nchi hiyo baada ya mijadala mingi kuhusu kugombea kwake katika uchaguzi wa Novemba 5 mwaka huu, na kumuunga mkono Kamala Harris, makamu wake kama mgombea wa kiti hicho.

Ikiwa ni miezi minne tu imebaki kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais wa Marekani, ushindani kati ya vyama viwili vya Demokratic na Republican kwa ajili ya kutwaa udhibiti wa Ikulu ya White House umeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimsingi.

Afisa mmoja wa Marekani amesema kuwa Biden alibadili mawazo yake ghafla kuhusu kuendelea kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu. Inasemekana kuwa Rais Biden alikasirishwa haswa na Nancy Pelosi, Spika wa zamani wa Congress, ambaye aliendesha kampeni ya kumlazimisha atoke kwenye kinyang'anyiro hicho cha kugombea tena urais wa Marekani.

Kama Biden angejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kabla ya kuanza chaguzi za utangulizi za Chama cha Demokratic, mrithi wake angekuwa na wakati wa kutosha wa kukusanya michango ya kumuwezesha kumshinda mgombea wa Republican, ambaye ni Donald Trump, lakini sasa zimesalia takriban siku 100 tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais, ambapo Chama cha Demokratic bado hakina mgombea wa kuchuana na Donald Trump katika uchaguzi huo.

Joe Biden akiwa na makamu wake  Kamala Harris ambaye huenda akachukua nafasi yake kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Demokratic

Kwa kuzingatia kuwa Biden tayari ametangaza uungaji mkono wake kwa Kamala Harris, huenda wanachama wengine wa Chama cha Democratic pia wakamuunga mkono, lakini pamoja na hayo viongozi wengine wa chama hicho kama vile Nancy Pelosi, Spika wa zamani wa Congress ya Marekani wamekataa kumuunga mkono. Licha ya hayo viongozi wakuu wa chama cha Democratic kama vile Bill Clinton na Hillary Clinton wametangaza kumuunga mkono Harris katika uchaguzi ujao wa urais. Hata hivyo, Harris ana upinzani mkubwa ndani ya chama hicho tawala.

Kuhusiana na hili, Alexander Ocasio Cortez, mjumbe wa chama cha Denocratic kwenye Congress anasema kuwa wale waliomshinikiza Joe Biden ajiondoe kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa 2024, hawana hamu ya kumtambulisha Kamala Harris kama mgombea mbadala wa  Biden. Pia katika kura nyingi za uchunguzi wa maoni, Kamala Harris hana nafasi nzuri kumliko Biden na hata yuko nyuma yake katika chunguzi hizo za maoni.

Dakika chache baada ya Joe Biden kutangaza kujiondoa kwenye kampeni za uchaguzi, Trump alimtaja kama rais mbaya zaidi katika historia ya Marekani, na kuongeza kuwa litakuwa jambo rahisi zaidi kumshinda Harris katika uchaguzi ujao kuliko Biden.

Kujiondoa Biden katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kuliibuliwa na kushindwa kwake katika mdahalo wa karibuni na Donald Trump, mgombea wa Republican ambapo wanachama wakuu wa Chama cha Democratic wamekuwa wakimshinikiza akae pembeni na kumuruhusu mtu mwingine kugombea kiti hicho.

Mdahalo wa kwanza wa rais Joe Biden na Donald Trump ulifanyika Juni 27, ambapo Biden alijiumauma midomo na kutamka maneno yasiyoeleweka, jambo liliwashangaza wengi na  kuanika peupe matatizo ya kiafya na kiakili yanayomkabili. Suala hilo na matatizo mengina kama hayo yanayomkabili mara kwa mara hadharani yamechukuliwa na wanachama wa Democratic na wachambuzi wengine wa mambo kuwa kengele ya hatari na hivyo kuwapelekea kuanza kutoa mashinikizo ya kumtaka ajiondoe katika mchakato wa kugemea tena kiti cha rais.

Wakati huo huo, matukio mengine kadhaa, haswa la kupigwa risasi Donald Trump, yameongeza umaarufu wake na kupunguza nafasi ya ushindi kwa Rais Biden.

 

Kujiondoa Rais Biden katika shindano la uchaguzi wa rais wa 2024 dhidi ya Trump

Jambo la kuzingatia kuhusu Kamala Harris ni kwamba yeye ni Makamu wa Rais Joe Biden na mrithi wa utendaji wake. Ikiwa Rais Biden amepoteza umaarufu wake mbele ya Wamarekani kama zinavyoonyesha chunguzi za kura ya maon, kutopendwa kwake huko kutamuathiri pia mrithi wake, hasa ikizingatiwa kuwa Harris hawezi kujitoa kwenye kivuli cha  Rais Biden.

Kwa ujumla, ni wazi kwamba kama Kamala Harris, akiwa mgombea wa Chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Marekani, anataka kuwa na fursa ya kumshinda Trump katika uachaguzi ujao, anapasa kuwasilisha mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto na matatizo sugu yanayoikabili Marekani kwa sasa katika miezi michache iliyobaki kabla ya uchaguzi. Miongoni mwa changamoto hizo muhimu ni suala la vita vya Ukanda wa Gaza na juhudi za kumaliza vita hivyo kwa lengo la kuvutia kura za wakosoaji wa siasa za serikali ya Biden katika uwanja huo.

Tags