Waziri Mkuu wa Bangladesh ajiuzulu, akimbia nchi,  jeshi kuunda serikali
(last modified 2024-08-05T12:33:52+00:00 )
Aug 05, 2024 12:33 UTC
  • Waziri Mkuu wa Bangladesh ajiuzulu, akimbia nchi,  jeshi kuunda serikali

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amejiuzulu na kutoroka nchi huku kukiwa na maandamano makali dhidi ya sera za serikali na utawala wake wa muda mrefu.

Hasina mwenye umri wa miaka 76 ameondoka leo Jumatatu katika mji mkuu Dhaka kwa helikopta ya kijeshi akiwa ameandamana na dada yake.

Vyombo mbalimbali vya habari vinasema amekimbilia India kutafuta hifadhi huko.

Maandamano hayo yalianza mwezi uliopita baada ya nchi hiyo kurejesha kanuni ya upendeleo ambayo inahifadhi zaidi ya nusu ya kazi zote za serikali kwa vikundi maalumu.

Maandamano hayo, hata hivyo, yaligeuka na kuwa maandamano makubwa ya kutaka kuondoka madarakani Hasina ambaye ametawala kwa miaka 15.

Takriban watu 300 wameripotiwa kuuawa katika maandamano hayo, ambayo ni mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo katika zaidi ya miongo mitano.

Maandamano hayo yaliyosababisha vifo vya watu wengi zaidi yalifanyika Jumapili, wakati takriban watu 94, wakiwemo maafisa 14 wa polisi, walipoteza maisha.

Mkuu wa Jeshi la Bangladesh Waker-Uz-Zaman

Baada ya Hasina kukimbia nchi, mkuu wa sasa wa jeshi la Bangladesh Waker-Uz-Zaman amesema ataunda serikali ya mpito.

Vikosi vya usalama viliunga mkono serikali ya Hasina wakati wote wa machafuko hayo. Siku ya Jumapili, hata hivyo, wakuu wa usalama walikataa kushirikiana na Hasina.

Kutoshirikiana kwao kumekuja baada ya Jenerali Ikbal Karim Bhuiyan, mkuu wa zamani wa jeshi, kuitaka serikali  kuondoa wanajeshi mitaani na kuruhusu maandamano yafanyike.

Tags