Aug 06, 2024 12:56 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka kukabidhiwa madaraka kwa amani nchini Bangladesh

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kuhamishwa madaraka kwa njia ya amani nchini Bangladesh, akitoa wito wa kuwajibishwa maafisa wa serikali ya nchi hiyo waliohusika na mauaji ya mamia ya watu na kujeruhiwa maelfu ya waandamanaji katika maandamano ya hivi karibuni dhidi ya serikali.

Volker Türk amesema kuwa uhamishaji wa madaraka kwa njia ya amani nchini Bangladesh ni muhimu na dharura kwa mujibu wa majukumu ya kimataifa ya nchi hiyo. Amesisitiza kuwa, mchakato wa kuhamisha madaraka nchini Bangladesh unapaswa kufanywa kwa njia ya uwazi na kuna udharura wa kutayarishwa mazingira ya kushirikisha watu wote kwa kuweka kando ghasia na utumiaji mabavu. 

Volker Türk ameashiria kauli ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Bangladesh kwamba baada ya kujiuzulu Waziri Mkuu, Sheikh Hasina Wazed, kutaundwa serikali ya mpito katika nchi hiyo, na kuongeza kuwa kuna udharura wa kuwepo dhamana ya uanzishwaji wa mfumo wa kidemokrasia na utawala wa sheria nchini Bangladesh haraka iwezekanavyo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amekariri wito wake wa kufanyika uchunguzi wa kina, usio na upendeleo na wa wazi kuhusu ukiukwaji wote wa haki za binadamu nchini Bangladesh, akisisitiza kwamba watu wote waliowekwa kizuizini kiholela lazima waachiliwe huru na wale wote wanaohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu wanapaswa kuwajibishwa.

Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina amejiuzulu na kutoroka nchi kufuatia maandamano makubwa ya wananchi dhidi ya sera za serikali na utawala wake wa muda mrefu.

Sheikh Hasina Wazed

Maandamano hayo yalianza mwezi uliopita baada ya nchi hiyo kurejesha kanuni ya upendeleo ambayo inahifadhi zaidi ya nusu ya kazi zote za serikali kwa vikundi maalumu.

Takriban watu 300 wameripotiwa kuuawa katika maandamano hayo, ambayo ni mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo katika zaidi ya miongo mitano.

Tags