Misimamo inayokinzana ya Ulaya katika vita vya Gaza: Kutoka vikwazo hadi mauzo ya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i117306
Licha ya madai yote ya nchi za Magharibi kuwa zinajaribu kuizuia Israel kuendeleza vita dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza, lakini nchi hizo hizo bado zinauuzia silaha utawala huo wa Kizayuni na hivyo kuendelea kuunga mkono na kuupa silaha za kila aina ili uendelee kuwaua kikatili watu wa Palestina na Lebanon.
(last modified 2024-10-09T11:30:52+00:00 )
Oct 09, 2024 11:30 UTC
  • Misimamo inayokinzana  ya Ulaya katika vita vya Gaza: Kutoka vikwazo hadi mauzo ya silaha

Licha ya madai yote ya nchi za Magharibi kuwa zinajaribu kuizuia Israel kuendeleza vita dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza, lakini nchi hizo hizo bado zinauuzia silaha utawala huo wa Kizayuni na hivyo kuendelea kuunga mkono na kuupa silaha za kila aina ili uendelee kuwaua kikatili watu wa Palestina na Lebanon.

Kuhusiana na hilo, Keir Starmer, Waziri Mkuu wa Uingereza amepinga vikali maombi na  matakwa ya kupiga marufuku kuuzia silaha utawala huo wa Kizayuni.

Ni karibu mwaka mmoja sasa ambapo sambamba na kuanza vita vya Gaza, utawala wa Kizayuni umekuwa ukiwachinja kinyama Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kiasi kwamba kufikia sasa, zaidi ya Wapalestina 41,000 wameuawa shahidi na maelfu ya wengine kujeruhiwa. Mbali na kufunga vivuko vyote, utawala huo haramu umezuia kuingia katika ukanda huo misaada ya kibinadamu na kutekeleza mipango ya kutaka kukifutilia mbali kizazi cha Wapalestina kwa kulipua kwa mabomu mazito hospitali na vituo vyao vya elimu.
Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina ni kubwa kiasi kwamba, katika miezi ya hivi karibuni nchi nyingi duniani, hata zile zinazounga mkono Wazayuni zimekuwa zikilaani jinai hizo. Maandamano hayo makubwa yamekuwa yakifanyika katika nchi nyingi za Ulaya ambapo wananchi wa nchi hizo wamezitaka serikali zao kusitisha mara moja misaada yao kwa utawala huo katili.

Mashinikizo hayo yamewafanya baadhi ya viongozi wa Ulaya wautake kidhahiri utawala wa Kizayuni uache kuwaua Wapalestina kwa kukubali usitishaji vita na kufanya mazungumzo ya amani. Espen Barth Eide, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway ametaja mateso na machungu wanayoyapitia  watu wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na Lebanon kuwa yasiyoelezeka na kutaka kuanzishwa mara moja usitishaji vita, kuheshimiwa sheria za kimataifa na kufanyika mazungumzo ya suluhisho la serikali mbili.

Nchi nyingine za Ulaya sambamba na kulaani jinai za utawala habithi wa Israel zimeahidi kuuwekea vikwazo na kuufutia mauzo ya silaha. Hii ni katika hali ambayo kwa hakika hakuna chochocje kinachofanyika kufikia lengo hilo, suala linalobainisha wazi siasa za undumakuwili na za hadaa za Wazungu. Isitoshe, wanaendelea kuunga mkono utawala huo haramu, kuuzia silaha na hata kuupa misaada mikubwa ya kifedha ili uendeleze jinai zake dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Uingereza ni miongoni mwa nchi zinazoidhaminia Israel mahitaji yake katika vita vyake vya jinai dhidi ya Wapalestina. Zara Sultana, mbunge wa Uingereza alisema siku chache zilizopita kuwa hakujawahi kusikika tena nara na kaulimbiu nyingi za kutetea uhuru wa taifa la  Palestina kama ilivyo hivi sasa. Lakini pamoja na hayo serikali ya Uingereza inaendelea kushiriki katika jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina kwa kukanusha kufanyika jinai hizo.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia silaha zilizopigwa marufuku kushambulia maeneo ya raia wa Lebanon na Ukanda wa Gaza.

Katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na kushadidi jinai za utawala wa  Israel, pamoja na kupanuka kwa wigo wa vita dhidi ya Lebanon, nchi nyingi za Ulaya zikiwa chini ya mashinikizo ya raia wao na baadhi ya mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu, yametaka kutazamwa upya sera za kuiunga mkono Israel, ikiwa ni pamoja na kupunguza au kusimamisha kabisa mauzo ya silaha kwa Tel Aviv. Pamoja na hayo, hali ya sasa ya vita na misimamo ya viongozi wa Ulaya inaonyesha wazi kuwa nchi za Magharibi zinaendelea kudumisha siasa zao za kuunga mkono kifedha na kijeshi utawala wa Israel na hudai kuunga mkono amani kwa lengo tu la kupunguza mashinikizo ya umma.

Katika muktadha huu, tunaweza kuashiria hapa msimamo wa David Lammy Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ambaye alikuwa akiishinikiza serikali iliyopita ichunguze jinai za utawala wa Kizayuni na ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu huko Ukanda wa  Gaza, lakini sasa si tu hajachukua hatua yoyote katika uwanja huo, bali serikali yake inaendelea kuiunga mkono na kuisaidia Israel katika kuendeleza jinai dhidi ya watu wasio na hatia.

Misimamo ya kundumakuwili ya nchi za Ulaya katika vita vya Gaza inaendelea katika hali ambayo utawala wa Israel kwa kutegemealea misaada chungu nzima kutoka Ulaya, unaendelea kufanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina. Ni wazi kuwa kufichuliwa jinai za Israel na kuongezeka mashinikizo ya wananchi ndiko kumewalazimisha Wazungu waanze kutamka maneno ya uongo kuwa wanataka kuuwekea utawala huo vikwazo vya silaha.