UN: Vita vimeathiri zaidi ya wanawake milioni 600 kote ulimwenguni
(last modified Mon, 28 Oct 2024 06:49:57 GMT )
Oct 28, 2024 06:49 UTC
  • UN: Vita vimeathiri zaidi ya wanawake milioni 600 kote ulimwenguni

Umoja wa Mataifa umesema kuwa, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 600 wameathiriwa na vita katika kona zote za dunia na hilo ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. Maafisa wakuu wa umoja huo wana wasiwasi kwamba ulimwengu umewasahau wanawake huku kukiwa na vilio vikubwa vya kukanyagwa zaidi haki za wanawake kwenye maeneo ya vita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema katika ripoti yake mpya kwamba, wanawake (na watoto) wameendelea kuwa wahanga wakuu kutokana na rekodi mpya ya migogoro ya silaha na unyanyasaji duniani.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa tathmini ya azimio la Baraza la Usalama lililopitishwa Oktoba 31, 2000, lililotaka wanawake washirikishwe kikamilifu katika mazungumzo ya amani. Amesema, lengo hilo bado liko mbali kufikiwa.

Wanawake nchini Sudan ni miongoni mwa wahanga wakuu wa vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi

 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, idadi ya wanawake waliouawa katika migogoro ya kivita iliongezeka maradufu mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka mmoja wa kabla yake; kesi zilizothibitishwa na Umoja wa Mataifa za unyanyasaji wa kingono zilipanda kwa asilimia 50 na idadi ya wasichana walioathiriwa na unyanyasaji wa kijinsia mwaka huo iliongezeka kwa asilimia 35. 

Katika mkutano wa siku mbili wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kujadili suala hilo, Sima Bahous, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kukuza usawa wa kijinsia lijulikanalo kwa jina la "UN Women," naye ameashiria kutozingatiwa sauti za wanawake katika kutafuta amani.

Ametoa mfano wa hofu waliyo nayo mamia ya maelfu ya wanawake huko Ghaza Palestina ambao amesema wanasubiri kifo wakati wowote na wanawake nchini Sudan ambao ni wahanga wakubwa wa unyanyasaji wa kijinsia; pamoja na wanawake waliokatishiwa ndoto zao wa nchi za Myanmar, Haiti, Kongo, eneo la Sahel la Afrika, Sudan Kusini, Ukraine na kwingineko na kuongeza kuwa, wanawake na wasichana milioni 612 ambao wameathiriwa na vita wanashangaa jinsi walivyosahaulika ulimwenguni.