Utafiti: Waislamu Ulaya waendelea kukabiliwa na ubaguzi
Waislamu barani Ulaya wameendelea kuandamwa na vitendo vya chuki na ubaguzi katika mataifa hayo yanayopigia debe uhuru wa kusema na kuabudu.
Ripoti zinaonyesha kuwa, vitendo vya kuratibiwa vya chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya vingali vinaendelea na moja ya matokeo yake ni kuimarika kwa tabia za kibaguzi na ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii ya Kiislamu katika bara humo.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni yanaonyesha kuwa, nusu ya Waislamu katika mataifa mbalimbali ya Ulaya walitusiwa au kubaguliwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwa uchache
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Shirika la Haki za Msingi la Ulaya (FRA) kuhusu ubaguzi dhidi ya Waislamu katika Umoja wa Ulaya, Waislamu nchini Ujerumani wamekumbwa na ubaguzi mkubwa zaidi wa rangi baada ya wenzao wa Austria.
Kushambuliwa misikiti na vituo vya kidini vya Waislamu, kuwanyanyasa Waislamu wanaovaa mavazi ya Kiislamu, na kukosekana usawa katika upataji ajira na elimu ni mifano hai ya mashinikizo yanayowaandama Waislamu katika nchi za Ulaya.