Trump: Nikichaguliwa tena kuwa rais naahidi "kuzitenganisha" Russia na China
Nov 02, 2024 06:04 UTC
Donald Trump, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican ameulaumu utawala wa Rais Joe Biden kwa kuukurubisha zaidi uhusiano kati ya Russia na China, na kuahidi kuwa atayatenganisha mataifa hayo mawili yenye nguvu za nyuklia akichaguliwa tena kuwa rais katika uchaguzi wa Novemba 5.
Trump ametoa ahadi hiyo katika mahojiano ya mubashara aliyofanyiwa na mwandishi wa habari wa Marekani Tucker Carlson mbele ya hadhara kubwa ya wafuasi wake huko Glendale, Arizona, ambapo alimshutumu pia Biden kwa kuharibu hadhi ya Marekani duniani.
Akimkosoa Biden kwa alichokiita kuchochea ushirikiano wa karibu kati ya Moscow na Beijing, rais huyo wa zamani wa Marekani amesema: “angalia nini wamefanya hawa wapumbavu. Wameruhusu Russia, China, Iran, Korea Kaskazini, na wengineo kukusanyika pamoja katika kundi moja" na akaongeza kuwa, mmoja wa maprofesa wake katika Kitivo cha Taaluma ya Fedha cha Wharton aliwahi kumwambia "jambo moja ambalo hutakiwi uruhusu kamwe litokee ni Russia na China kuungana."
Katika mahojiano hayo,Trump ameendelea kusema bila kufafanua: “tuliwaunganisha kwa sababu ya mafuta. Biden aliwaunganisha. Ni aibu,” na akasisitiza kwa kusema: "itanibidi niwatenganishe, na nadhani ninao pia uwezo wa kufanya hivyo."
Russia na China ni wanachama wa miungano kadhaa ya kikanda, ikiwa ni pamoja na BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai. Nchi hizo mbili zimeuelezea uhusiano wao kuwa ni ushirikiano wa kimkakati na zimeungana dhidi ya sera ya kujichukulia hatua za "upande mmoja" ya Marekani katika uga wa kimataifa.
Aidha, Beijing imekataa kujiunga na vikwazo vya kiuchumi vya Magharibi vilivyowekwa dhidi ya Russia kutokana na mzozo wa Ukraine.
Mwezi uliopita, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema, nchi hiyo na wanachama wengine wa BRICS wamehamia kwenye utumiaji wa sarafu zao za taifa katika 65% ya biashara baina yao.
Mapema mwaka huu, kiongozi huyo alibainisha pia kwamba, 90% ya miamala kati ya Russia na mshirika wake mkubwa wa kibiashara China, inafanywa kwa kutumia sarafu za taifa za nchi hizo mbili..../