Waingereza waandamana 'Siku ya Balfour' kulaani jinai za Israel Gaza
(last modified Sun, 03 Nov 2024 06:16:48 GMT )
Nov 03, 2024 06:16 UTC
  • Waingereza waandamana 'Siku ya Balfour' kulaani jinai za Israel Gaza

Makumi ya maelfu ya watu nchini Uingereza waamemiminika mabarabarani mjini London kushiriki maandamano ya kupinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza katika Siku ya Balfour, kumbukizi ya kila mwaka ya kuadhimisha nafasi ya Uingereza katika kuasisiwa utawala wa Kizayuni mwaka 1917.

Waandamanaji kutoka matabaka mbalimbali ya watu, mataifa, na dini tofauti walikusanyika mbele ya Ofisi ya Jumuiya ya Madola ya Kigeni ya Uingereza (FCDO) jana Jumamosi, kushiriki maandamano hayo.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, waandamanaji walisikika wakipiga nara dhidi ya Israel, huku wakitaka kukomeshwa uungaji mkono wa London kwa utawala huo wa Kizayuni.

Huku wakitoa wito wa ukombozi wa Palestina na kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na Lebanon, waandamanaji hao waliandamana na kukusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani mjini London. Kadhalika wameikosoa Marekani kwa nafasi yake katika kushadidi mgogoro wa kibinadamu huko Gaza na Lebanon kwa uungaji mkono wake kamili kwa utawala wa Kizayuni.

Waandamanaji UK watangaza mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina

Ikumbukwe kuwa, miaka 107 iliyopita katika siku inayosadifiana na tarehe Pili Novemba mwaka 1917, lilitolewa Azimio la James Balfour. Tangazo hilo lililotolewa na Arthur James Balfour, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Uingereza liliandaa uwanja wa kuasisiwa utawala haramu wa Israel huko katika ardhi za Palestina zilizokuwa chini ya wakoloni wa Uingereza.

Katika mahojiano na shirika la habari la IRNA, Ben Jamal, Mkurugenzi wa Kampeni ya Mshikamano na Palestina (PSC) amesema kuwa, serikali ya Uingereza imekataa kuzitambua jinai za utawala wa Kizayuni wa Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari.