Utafiti: Idadi ya wagonjwa wa kisukari duniani imeongezeka
Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa, idadi ya watu wazima wanaougua kisukari duniani kote imeongezeka maradufu katika miongo mitatu iliyopita, huku ongezeko kubwa likishuhudiwa katika nchi zinazoendelea.
Utafiti huo uliofanywa na jarida la The Lancet unaonyesha kuwa, tatizo la kisukari limeathiri karibu asilimia 14 ya watu wazima duniani kote kufikia mwaka 2022, ikilinganishwa na asilimia saba mwaka wa 1990. Kwa mujibu wa utafiti huo, zaidi ya watu milioni 800 duniani sasa wanaugua kisukari.
Wataalamu wanasisitiza kuwa unene kupita kiasi ni sababu kubwa inayochangia kisukari aina ya 2 huku pengo la kutibu ugonjwa huo baina ya nchi tajiri na maskini pia likiongezeka.
Kisukari ni miongoni mwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaua watu zaidi ya milioni moja kila mwaka - na unaweza kumpata mtu yeyote.
Miongoni mwa dalili zake ni: Kuhisi kiu sana, kukojoa zaidi ya kawaida hasa nyakati za usiku, kujisikia kuchoka sana, kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri, kutoona vizuri na kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake.