Ireland yajiunga na kesi ya Afrika Kusini ICJ dhidi ya Israel
Serikali ya Ireland imetangaza kujiunga na kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya utawala haramu wa Israel unaotenda jinai dhidi ya Wapalestina.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ireland ametangaza kuwa, nchi hiyo imejiunga rasmi na kesi ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.
"Michael Martin," Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, amesema kuwa serikali ya Ireland imekubali kushiriki katika kesi ambayo Afrika Kusini iliwasilisha kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya Israel chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.
Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana 2023, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu dhidi ya utawala wa Kizayuni kutokana na utawala huo kukiuka makubaliano ya kupigwa marufuku jinai za mauaji ya halaiki.
Mwezi uliopita, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa waranti wa kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Gallant baada ya kuwafungulia mashtaka ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Ghaza, ambako utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kinyama na kufanya mauaji ya kimbari tangu mwezi wa Oktoba mwaka jana.