Ujio wa Trump; Marekani yawakamata na kuwafukuza mamia ya wahamiaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121856-ujio_wa_trump_marekani_yawakamata_na_kuwafukuza_mamia_ya_wahamiaji
Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House ya Marekani amefichua kuwa, katika wiki ya kwanza ya urais wa Donald Trump, wahamiaji haramu 538 wamekamatwa na kuzuiliwa, huku mamia ya wengine wakifukuzwa nchini.
(last modified 2025-01-25T02:56:44+00:00 )
Jan 25, 2025 02:56 UTC
  • Ujio wa Trump; Marekani yawakamata na kuwafukuza mamia ya wahamiaji

Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House ya Marekani amefichua kuwa, katika wiki ya kwanza ya urais wa Donald Trump, wahamiaji haramu 538 wamekamatwa na kuzuiliwa, huku mamia ya wengine wakifukuzwa nchini.

Karoline Leavitt, Katibu wa Habari wa White House amesema kufukuzwa huko ni sehemu ya "Operesheni kubwa zaidi ya kufurusha (wahamiaji) katika historia".

Amedai kuwa, watu waliokamatwa ni pamoja na wanachama wa magenge yenye silaha. Moja ya ahadi kuu za kampeni za Donald Trump wakati wa uchaguzi wa urais wa 2024 ilikuwa kuzuia wahamiaji haramu kuingia Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ikulu ya Marekani, katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Biden, zaidi ya wahamiaji haramu milioni 8 wameingia Marekani, huku milioni 6.7 wakiingia kupitia mpaka wa kusini.

Ingawaje matamshi ya Trump dhidi ya uhamiaji yalilenga zaidi wahamiaji haramu, lakini katika siku ya pili ya utawala wake, alitia saini amri ya utendaji ya kuwafukuza wanafunzi wahamiaji halali wanaodaiwa 'kuwaonea huruma' maadui wa Israel.

Habari zaidi zinasema kuwa, safari za ndege za wakimbizi zilizotazamiwa kuwasili Marekani karibuni zimefutwa, huku askari wakitumwa kwenye mpaka wa kusini, sambamba na mamlaka husika kuidhinishwa kuwakamata wahamiaji ndani au karibu na shule na makanisa.