Marekani kuipa Israel mabomu 1,800 aina ya MK-84
Washington imesema mabomu 1,800 ya MK-84 yaliyohifadhiwa Marekani yatasafirishwa na kupelekewa utawala wa Kizayuni wa Israel katika siku chache zijazo.
Ikulu ya White House imeiagiza Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon kuondoa kizuizi cha upelekaji wa mabomu hayo yenye uzani wa pauni 2,000 kwa Israeli, kulingana na maafisa watatu wa Israeli wanaozungumza na Axios.
Uamuzi wa Rais Joe Biden wa kusitisha usafirishaji wa mabomu hayo mwezi Mei mwaka jana uliibua mgogoro mkubwa katika uhusiano wa Marekani na Israel, wakati wa vita dhidi ya Gaza vilivyodumu kwa zaidi ya miezi 15.
Habari zaidi zinasema kuwa, Pentagon iliifahamisha serikali ya Tel Aviv kuhusu kuondolewa marufuku hiyo siku ya Ijumaa.
Utawala wa Biden ulidai kwamba, eti una wasiwasi juu ya matumizi ya Israel ya mabomu hayo aina ya MK-84 dhidi ya Gaza yenye wakazi wengi yangelisababisha vifo vingi vya raia.
Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel, Benjamin Netanyahu na wafuasi wake huko Israeli na Marekani walitumia uamuzi wa Biden kudai, kimakosa, kwamba Marekani ilikuwa imeiwekea Israel vikwazo vya silaha.